MECHI YA SIMBA NA YANGA KUPIGWA NJE YA DAR
Yanga wanachoangalia ni mapato tu na sasa wanapanga hoja zao ambazo TFF inazisubiri pale ofisini Karume, Ilala.
KAMA Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) likikubaliana ushawishi wa Yanga, hakuna namna mechi ijayo ya watani wa jadi itapigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Oktoba 28 mwaka huu.
Yanga wanachoangalia ni mapato tu na sasa wanapanga hoja zao ambazo TFF inazisubiri pale ofisini Karume, Ilala. Mabingwa hao wa Ligi Kuu wamebaini wakicheza na Simba kwenye Uwanja wa Uhuru hawatapata mshiko wa maana hivyo wameandaa maombi maalumu ya kuupeleka mchezo huo Mwanza ambako wana rekodi nzuri pia dhidi ya watani zao Simba.
Takwimu zinaonyesha kuwa Uwanja wa Uhuru una uwezo wa kubeba mashabiki 23,000 walioketi wakati ule wa Kirumba unabeba mashabiki 35,000 hivyo mapato huenda yakaongezeka maradufu.
Yanga pia imekuwa na bahati na Uwanja wa Kirumba kwani mwaka 2005 ilipata ushindi mkubwa dhidi ya Simba uwanjani hapo tena baada ya kunyanyasika kwenye michezo mingi. Yanga ilikuwa imecheza miaka mitano bila ushindi dhidi ya Simba.
Afisa Habari wa Yanga, Dismas Ten alisema wako kwenye mchakato na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Mkwasa kuona namna ya kuishawishi bodi ya Ligi mchezo huo uhame na wana hoja za msingi.
“Sisi ndiyo wenyeji na tutakuwa na mgawo mkubwa hivyo lazima tutazame namna ya kupata fedha nyingi kutoka kwenye mchezo huo,” alisema Ten ambaye kwa sasa anatengeneza App ya Yanga itakayowafanya kujitangaza kimataifa.
“Katibu ametaka kuona hoja tulizonazo na kama tunaweza kupata ruhusa. Kama atakubali tutapeleka maombi ya kuhamishia mchezo huo Mwanza. Hii itatusaidia kupeleka burudani nje ya Dar es Salaam lakini pia kuongeza mapato.
“Kiuhalisia uwanja wa Kirumba ni mkubwa kuliko ule wa Uhuru, hivyo tunaweza kupata fedha nyingi zaidi tukicheza Mwanza,” alifafanua ofisa habari huyo wa zamani wa Mbeya City.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau alisema wanaweza kuwaruhusu Yanga kufanya hivyo endapo watajiridhisha kuwa watapata fedha nyingi zaidi Mwanza kuliko wakicheza Dar es Salaam.
“Kwa upande wangu naona wakicheza hapa Dar es Salaam watapata fedha nyingi zaidi kwa kuwa bei ziko juu, eneo la tiketi za 30,000 pia ni kubwa kuliko Mwanza. Sidhani kama uwezo wa uwanja wa Kirumba na Uhuru unatofautiana sana,” alisema Kidau.
“Wao wawasilishe maombi yao Bodi ya Ligi kisha tutatazama hoja zao, tutajaribu kuwaelewesha maana ukienda Mwanza hata gharama zinakuwa kubwa kwani timu zitalazimika kusafiri na kuweka kambi kule.
“Kuna vitu vingi vinaongezeka lakini yote kwa yote tusubiri kwanza maombi yao, ni jambo linalowezekana pia,” alifafanua Kidau ambaye amewahi kuwa kocha wa AFC ya Arusha.
No comments