LAPF yatoa Dola 3.9 milioni kiwanda cha nyama Morogoro
Morogoro. Kwa mara nyingine, Mfuko wa Pensheni wa LAPF umewekeza mkoani hapa baada ya kutoa Dola 3.9 milioni za Marekani (zaidi ya Sh7.8 bilioni) kwenye kiwanda cha usindikaji nyama cha Nguru.
Uwekezaji huo ni baada ya kujenga kituo bora zaidi nchini cha mabasi ya kwenda mikoani mjini Morogoro. Kwa kiasi cha fedha kilichotolewa, LAPF itamiliki asilimia 39 wakati wabia wenza; Kampuni ya Eclipse Investments itakuwa na asilimia 46 na kampuni ya Busara Investments asilimia 15.
Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Eliud Sanga amesema mfuko umejiridhisha kuhusu usalama wa rasilimali za wanachama na umetambua fursa za uwekezaji katika kiwanda hicho.
“Kinatarajiwa kuanza uzalishaji Januari. Ng’ombe 300 na mbuzi 2,000 watachinjwa kila siku na bidhaa itakayozalishwa kusafirishwa nje ya nchi na hasa Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati,” amesema.
Si tu biashara hiyo italeta fedha za kigeni, bali itaongeza ajira kwa vijana kutoka maeneo tofauti nchini na kutoa soko la uhakika kwa maelfu ya mifugo ya wafugaji waliopo mkoani Morogoro na Tanzania kwa jumla.
Sanga ameutaka uongozi wa mkoa kujiandaa kisaikolojia kuhudumia ongezeko la watu litakalokuwepo siku zijazo baada ya kiwanda kuanza uzalishaji.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari amesema uwekezaji unaoendelea kufanyika utaleta ajira nyingi kwa vijana.
“Uwekezaji huu utawaamsha vijana kuchangamkia fursa zilizopo,” amesema.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Zubair Corporation ambayo ni kampuni mama ya Eclipse Investments ambayo ni mbia, Cerusiri Badrinath amesema wamewekeza nchini baada ya kuridhishwa na mazingira yaliyopo na washirika wao.
No comments