Breaking News

KIJANA WA MIAKA 18 ASIMULIA ALIVYOWATEKA WATOTO WANNE ARUSHA


Matukio ya utekaji watoto mjini Arusha yameanza kupata mwelekeo wa ufumbuzi baada ya kijana wa miaka 18 kukiri kuwateka watoto wanne alipokamatwa katika mji wa Katoro wilayani Geita alikofanya tukio jingine la utekaji.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari akiwa chini ya ulinzi wa polisi jana, kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Samson Petro alisema watoto wawili aliwarudisha kwa wazazi wao baada ya kupewa Sh300,000.

Alisema wengine wawili aliwatelekeza mtaani baada ya wazazi wao kutotoa kiasi cha fedha walichotakiwa kumpa.

Samson alisema alianza ‘shughuli’ hiyo ya utekaji watoto kutokana na mahitaji ya fedha na kwamba, aliacha shule akiwa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lutozo iliyopo Katoro.

“Naishi na wazazi wangu, lakini nao ni masikini, nilifanya hivi ili nipate fedha na nilikuwa nikimchukua mtoto naandika ujumbe kwenye karatasi, naandika na namba ya simu napeleka karibu na familia ili wanitafute,” alisema Samson.

Awali, kamanda wa polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema walimkamata kijana huyo katika nyumba ya kulala wageni ya Shitungulu iliyopo mjini Katoro juzi saa mbili usiku.

Mwabulambo alisema polisi mkoani Geita kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha walifanya uchunguzi na kubaini mtuhumiwa alikuwa Katoro.

Alisema walipata taarifa za kutekwa Justin Ombeni (2) Septemba Mosi nyumbani kwao katika eneo la Shilabela ambako mtuhumiwa alikwenda na kuwakuta watoto wanne wakicheza nyuma ya nyumba.

Alisema aliwagawia pipi na kuondoka na Justin. Kamanda huyo alisema polisi ilipata taarifa kuwa kijana huyo yupo chumba namba 103 katika nyumba hiyo ya wageni ambako waliweka ulinzi kuizunguka.

Alisema walipoingia katika chumba hicho walimkuta akiwa na
mtoto huyo. Mwabulambo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Ombeni Mshana ambaye ni baba wa Justin alisema mtekaji huyo alimpatia ujumbe mtoto wa jirani uliomtaka kutuma Sh4 milioni na walipokuwa wakiwasiliana na mtuhumiwa alishusha kiwango hadi Sh1 milioni.

Alisema polisi walimtahadharisha kwamba asitume fedha hizo.Kamanda Mwabulambo alisema tukio la kutekwa Justin ni la pili katika kipindi cha miezi minne baada ya mwingine kutekwa.

Kesi kuhusu tukio hilo la kwanza inaendelea mahakamani baada ya mtoto kupatikana.

Katika hatua nyingine, kikosi kilichoundwa na wananchi mkoani Arusha kikiongozwa na mwenyekiti wa Mtaa wa Olkerian, Kata ya Olasiti, Daudi Safari na familia za watoto wawili waliotekwa kimewakamata watuhumiwa wawili na kuwafikisha polisi.

Watoto hao ambao bado hawajapatikana ni Moureen David (6) anayesoma darasa la kwanza shule ya msingi Lucky Vincent na Ikram Salim (3).

Wakizungumza jana nje ya kituo kikuu cha polisi Arusha baada ya kuwafikisha kituoni watuhumiwa hao, Safari na wazazi wa watoto hao, David Njau na Salim Kassim walisema kwa nyakati tofauti wameanzisha msako baada ya
kuona siku zinakwenda bila watoto kupatikana.

Moureen alitekwa Agosti 21 saa 11 jioni akiwa anacheza nyumbani kwao eneo la Olasiti, wakati Ikram alitekwa Agosti 26 saa 12 jioni akiwa anacheza na watoto wenzake nyumbani kwao, Burka - Olasiti.

Safari alisema wamemkamata mtu mmoja (jina linahifadhiwa)
ambaye simu yake ilitumiwa na watekaji kuomba fedha kwa mzazi wa Ikram Salim.

Alisema pia wamemkamata wakala wa fedha wa kampuni moja ya simu (jina tunaihifadhi) aliyetoa Sh300,000 kwa watekaji baada ya fedha kutumwa na mzazi wa Ikram.

Imeelezwa kuwa wakala huyo amekamatwa kwa kuwa fedha hizo zilitolewa pasipo kuorodheshwa popote na mpokeaji hakuonyesha kitambulisho chochote.

Akizungumzia operesheni hiyo, Njau alisema hawatapumzika mpaka watoto wao wapatikane.

Alisema ufuatiliaji walioufanya kupitia minara ya kampuni za simu unaonyesha wahusika walikuwa eneo la Kwa Mrombo jijini Arusha walipopiga kuomba Sh4.5 milioni ili wamwachie Doreen na kiasi kingine kama hicho kwa ajili ya Ikram.

Watekaji hao kupitia ujumbe waliotuma nyumbani kwa Njau walidai kama wasipopewa fedha wangempoteza mtoto huyo japokuwa hawana nia hiyo.

Kassim Salim ambaye ni babu wa Ikram alisema, “tunaendelea kuomba msaada zaidi kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na vyombo vya dola watusaidie tuwapate watoto wetu.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema juzi kuwa watu watatu wanashikiliwa wakihusishwa na tukio hilo akiwapo dereva wa bodaboda mkazi wa Olasiti aliyetumwa kuwarejesha watoto wawili waliokuwa wametekwa.

Matukio ya utekaji yalianza kuibuka Agosti 21 baada ya kutekwa watoto wanne. Watoto wawili Ayoub Fred na Bakati Selemani wakazi wa eneo la FFU, kata ya Murieti jirani na kata ya Olasiti walirejeshwa

No comments