Katibu wa Mbunge Ashangazwa na Kamatakamata ya Polisi
Katibu wa Mbunge wa Tarime Vijijni John Heche, Mrimi Zabloni amesema analishangaa Jeshi la Polisi nchini kwa kukamata watu wanaokusanyika kumuombea Tundu Lissu na kuruhusu matamasha yanayofanyika usiku kucha huku viongozi wa mikoa wakishiriki.
Mrimi amefunguka hayo wakati akizungumza kwa njia yasimu na Mwandishi wa EATV na kusema kwamba anasikitisha na vitendo vinavyofanywa na jeshi la polisi kukataza mikusanyiko ya wanachadema badala ya kuipa ulinzi.
"Kuna vitu hawa askari polisi wetu wanafanya vya kushangaza, kuna matamasha mengi yanafanyika usiku na viongozi wa mikoa wanashiriki lakini maombi ya Lissu yanayofanywa mchana kweupe wanayapinga, sijui tunaelekea wapi. Kati ya matamasha ya usiku na maombi yapi yanahatarisha amani? Wenzetu Kenya jana wamefika hadi hospitalini na kufanya ibada kwa ajili ya kumuombea Lissu kwa nini hatujifunzi kutoka huko? alisisitiza kwa njia ya kuhoji.
Aidha Mrimi amewataka watu kutohusisha tukio la Tundu Lissu kama mtaji wa siasa kwa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) na kwamba harakati zinazofanywa na vijana hao ni kuhakikisha wanatoa hisia zao juu ya matatizo aliyoyapata mwanasheria wao.
Amesema kuwa wanachokifanya Bavicha siyo siasa bali wanatumia uhuru wa Katiba na kwa mujibu wa sheria ya vyama vingi nchini kwani wanaruhusiwa kuzungumza na hata kuandamana ili kutoa hisia zao kwa mambo yanayoendelea nchini.
"Wanaosema Bavicha wanamtumia Lissu kama mtaji wa kisiasa ni mtazamo wao tu, kwani naamini wanafanya kazi kwa mujibu wa heria na katiba hayo mengine ni hila tu. Naamini wamekumbwa na matatizo mengi viongozi kupotea, misukosuko ya viongozi wa chama lakini pia hata mauaji yaliyowahi kutokea kwa viongozi na shambulio la Lissu kwa hiyo ni haki yao kama vijana kupaza sauti kukemea" Mrimi aliongeza
No comments