JAFO AWATAKA WAKUU WA WILAYA KUITUMIA VIZURI SHERIA YA KUWEKA NDANI WATU
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amewatakaa Wakuu wa Wilaya kuitumia vizuri sheria ya kumuweka mtu ndani kwa saa 48 pasipo uonevu wowote.
Jafo ameitoa kauli hiyo Mjini Dodoma alipokuwa akifunga mafunzo ya Uongozi ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Shinyanga na Dar es Salaam, Yalioanza Septemba 11, mwaka huu.
"Fanyeni kazi kwa kufuata mipaka yenu ya kazi, kwani ndilo jambo pekee litakalo waepusha na migogoro katika maeneo yenu ya kazi," amesema Jafo.
Amesema , viongozi hao wanapaswa kufanya kazi pasipo kumuonea au kumpendelea mtu kwa namna yoyote ile, bali wakawe mifano kwa kujenga uhusiano mzuri na watumishi wanao waongoza pamoja na wananchi.
Jafo amewataka kwenda kufanya mabadiliko katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vita dhidi ya rushwa na dawa za kulevya, usimamizi wa miradi ya maendeleo,matumizi ya mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali pamoja na kusimamia uwajibikaji wa watumishi wa umma.
Wakati wakiendelea na mafunzo hayo, Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi John Kijazi amewatembelea Wakuu hao wa Wilaya na kuwapa miongozo ya utendaji kazi pamoja na mipaka ya kazi yao ili kuepuka migogoro katika maeneo yao ya kazi.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo kutoka Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo alizitaja mada walizofundishwa viongozi hao kuwa ni pamoja na muundo wa Serikali, namna ya kumbadili kiongozi, utunzaji wa nyaraka na siri za Serikali, manunuzi, matumizi sahihi ya vyombo vya usalama, usalama wa nchi pamoja na mambo ya uchaguzi.
No comments