GEITA MAMBO BADO MAGUMU MADIWANI WAWILI RUMANDE
Geita. Madiwani wawili kuwekwa rumande na kuvunjwa kioo cha gari la halmashauri ni miongoni mwa matukio yaliyotikisa mjini Geita, polisi walipowadhibiti wawakilishi hao wa wananchi waliofunga barabara kushinikiza malimbikizo ya malipo ya ushuru.
Mbali ya madiwani hao, pia kuna wananchi wanaoshikiliwa na polisi mmoja kati yao akiwa amejeruhiwa mguuni.
Madiwani wa halmashauri mbili za Wilaya ya Geita jana walifunga barabara ya kuingia katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), wakishinikiza kulipwa Dola 12 milioni za Marekani zinazotokana na ushuru wa huduma kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.
Hata hivyo, GGM ilisema suala hilo lifikishwe mahakamani kwa kuwa linahusu sheria mbili zinazopingana ambazo zote zimetungwa na Bunge.
Madiwani hao walifunga barabara zinazoingia mgodini jana kuanzia saa 10:30 alfajiri wakizuia magari yanayoingia na kutoka ndani ya mgodi, hivyo kusababisha shughuli mgodini kusimama kutokana na wafanyakazi kutoingia kazini.
Wakishirikiana na wananchi, madiwani hao waliweka kambi kwenye lango kuu la kuingia mgodini, la kuingia uwanja wa ndege uliopo ndani ya mgodi na kwenye eneo la Nungwe kilipo chanzo cha maji kutoka Ziwa Victoria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo saa nne asubuhi aliwataka madiwani na wananchi watawanyike na kurudi nyumbani bila mafanikio hivyo kulazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Waliokamatwa na polisi ni makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Hadija Said ambaye alianguka akiwakimbia askari.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Costantine Morandi alisema jana kuwa mwingine anayeshikiliwa na polisi ni Martin Kwilasa ambaye ni diwani wa Bung’wangoko.
Katika vurugu hizo zilizoshuhudiwa na mwandishi wa Mwananchi, gari alilokuwa amepanda makamu mwenyekiti wa halmashauri, Said lilivunjwa kioo na polisi. Dereva wa gari hilo, Sylvester Mahendeka akitoa maelezo kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Geita, Ally Kitimbu baada ya kioo cha upande wake kuvunjwa alisema akiwa amesogeza gari pembeni kumsubiri Said alifika askari aliyemtaka alitoe eneo hilo.
Said alisema alimweleza askari huyo kwamba anamsubiri makamu mwenyekiti ndipo alipokipiga kwa kirungu kioo na kukivunja.
Baada ya tukio hilo, polisi waliimarisha ulinzi kwenye maeneo ya Nungwe uliko mradi wa kusambaza maji mgodini, eneo la uwanja wa ndege na geti la kuingia mgodini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda Mwabulambo alithibitisha kukamatwa kwa madiwani hao akisema pia kuna mwananchi mmoja ambaye alijeruhiwa.
Alisema kitendo kilichofanywa na madiwani hao ni uvunjifu wa sheria na hawezi kuvumilia, hivyo wanaendelea kuwafuatilia wengine ambao uchunguzi unaonyesha walihusika kuhamasisha madiwani kuvunja sheria.
Chanzo cha mgogoro
Katika kikao cha juzi kilichohudhuriwa na madiwani wa halmashauri hizo, mwakilishi wa GGM, wakurugenzi wa halmashauri zote mbili na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi walitangaza kuzuia magari ya mgodi kwa kufunga barabara jana na kufunga maji yanayoingia mgodini kutoka Ziwa Victoria.
Hatua hiyo inatokana na mgogoro ambao halmashauri zinadai kulipwa na GGM Dola 12 milioni za Marekani zinazotokana na ushuru wa huduma kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.
Madiwani wanasema fedha hizo ni haki yao kwa mujibu wa sheria kwa kuwa mgodi ulipaswa kulipa ushuru wa huduma wa asilimia 0.3, lakini hawakulipa na badala yake walilipa Dola 200,000 kwa mwaka tangu 2004 hadi 2013 kinyume cha sheria.
Hata hivyo, meneja uhusiano ya jamii kutoka mgodi wa GGM, Manase Ndoroma alisema kinachosababisha mgogoro kati ya pande hizo ni kupingana kwa sheria ambazo zote zimetungwa na Bunge.
Alisema sheria ya madini iliwaruhusu kulipa Dola 200,000 kwa mwaka, huku sheria ya baraza la madiwani ikiwa imepitisha malipo ya asilimia 0.3 jambo linalosababisha mgogoro na suluhisho pekee ni kwenda mahakamani.
Halmashauri hizo na GGM zimekuwa kwenye mgogoro kwa zaidi ya mwezi sasa kutokana na madai ya fedha hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kapufi ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama akizungumza juzi kwenye kikao baada ya madiwani kutangaza kufunga barabara alisema atakachofanya ni kusimamia amani na kuhakikisha hakuna mali itakayoharibika kutokana na mgogoro huo.
Makubaliano yafikiwa
Baada ya kupigwa mabomu na kutawanyika madiwani walikutana kwenye ukumbi wa mkutano wa halmashauri ya wilaya, wakimtuhumu kamanda wa polisi wa mkoa kuwa amewatukana na ametumia nguvu kubwa kuwadhibiti.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake, mwenyekiti wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Elisha Lupuga alisema kitendo cha polisi kutumia nguvu kuwatawanya na kuwaita madiwani wa CCM viherehere si cha kiungwana na hawapo tayari kufanya naye kazi.
Lupuga alimtaka Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma kupeleka jambo hilo bungeni.
Akizungumza katika kikao hicho, Msukuma alisema wanachodai ni mapato ya halmashauri hivyo wanashangazwa na nguvu kubwa iliyotumiwa na polisi.
Mkuu wa Wilaya Kapufi alilazimika kumuita Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga aliyefika kuzungumza na madiwani hao akiwaomba kutumia hekima na busara katika jambo hilo.
“Uzee ni dawa, matukio kama haya yanahitaji kutumia hekima na busara kwa manufaa ya wananchi. Shughuli za kijamii haziwezi kusimama kwa kuwa mnachofanya ni kinyume cha sheria za nchi,” alisema Kyunga.
Aliwasihi madiwani kurudi nyumbani kuendelea na shughuli zao kwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na kamishna wa madini wameridhia kwenda kuwasikiliza na kutafuta muafaka wa mgogoro huo Jumatatu.
No comments