Breaking News

CHADEMA YAIBUA MAZITO ZIDI YA BUNGE

Chadema imedai Bunge limepata fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina kwa kukiuka Katiba na sheria

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibua tuhuma nzito dhidi ya Bunge kikidai kutumia njia zilizokiuka Katiba na sheria katika utaratibu wa upatikanaji wa Sh9 bilioni kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina.

Tuhuma hizo zimeelekezwa kwa Wizara ya Fedha na Mipango na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah.

Dk Kashilillah anadaiwa kuwasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa Hazina na kwa Waziri wa Fedha akiomba fedha kwa ajili ya kugharimia bajeti ya ziada. Barua hizo anadaiwa kuziwasilisha kati ya Juni 21 na Agosti 15.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji leo Septemba 6 akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 ibara ya 135(2) inaeleza fedha zitakazowekwa katika Mfuko wa Hazina ni zilizotajwa na sheria na kwamba, zitumike kwa shughuli maalumu au ziwekwe katika mfumo mwingine kwa ajili ya matumizi maalumu.

Pia, kifungu cha 31 cha Sheria ya Uendeshaji wa Bunge ya mwaka 2008 kinaeleza fedha zote za uendeshaji wa Bunge zimewekwa katika mfuko maalumu wa Bunge na msimamizi mkuu wa fedha hizo ni Katibu wa Bunge kama ilivyoelezwa katika vifungu vya (2) na (3).

“Kuna Sh2.5 bilioni ambazo zitatolewa ili kulipia posho ya jimbo ya Juni lakini mwaka wa 2016/17 Bunge liliidhinisha bajeti ya Sh92 bilioni za mishahara, Sh68.2 bilioni za matumizi mengineyo na Sh7 bilioni za matumizi ya maendeleo ya ndani. Sasa fedha hizo inaomba kwa utaratibu upi? Tatizo si kuomba fedha, bali ni mazoea ya ukiukwaji wa Sheria na Katiba,” amesema.

Dk Mashinji amesema fedha zilizotolewa kama bajeti ya ziada zilitumika kwa malipo ya posho ikiwemo ya jimbo ya Mei, ya kujikimu ya Juni, ya vikao vya Mei na Juni, posho ya saa nyingi kwa watumishi ya Mei na ya kikao cha kamati maalumu, zote zikiwa kwa mwaka huu.

Amesema uvunjaji wa sheria katika Serikali ulianzia katika nafasi za uteuzi wa kada wa CCM kuwa wakurugenzi wa halmashauri ambao hutumika katika nafasi za uwakilishi wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (Nec) ngazi ya wilaya.

Dk Mashinji amesema ukiukwaji huo ulionekana tena katika ununuzi wa ndege za Bombardier.

“Kwa hiyo tunaliomba Bunge kama msimamizi mkuu wa Serikali lijitafakari. Uimara wa Bunge si kupambana na wabunge wa upinzani tu, kuwafukuza na kuzuia hoja za upinzani, kushindwa kusimamia Bunge ni udhaifu mkubwa na haya yote yanafanyika kwa kukosekana Katiba mpya ya wananchi,” amesema Dk Mashinji.

Katika kutafuta ufumbuzi wa dosari hiyo, amesema Chadema kupitia mbunge na Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde atawasilisha hoja bungeni inayoshinikiza uendeshaji za mchakato wa Katiba Mpya.

Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashantu Kijaji amesema Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 kifungu cha(41)(7) inamruhusu Waziri wa Fedha kufanya uhamisho wa fedha kutoka fungu moja kwenda lingine ndani ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka husika.

Dk Kijaji amesema licha ya kutokuwa na taarifa rasmi kuhusu tuhuma hizo, ni upotoshaji kusema Waziri wa Fedha hana mamlaka moja kwa moja katika ubatilishaji matumizi ya fedha za Serikali.

Ufafanuzi wa Bunge

Katibu wa Bunge, Dk Kashilillah amesema hakuna kifungu cha sheria kilichokiukwa katika utaratibu wa fedha hizo.

Amesema kilichofanyika ni uhamishaji wa fedha kutoka fungu moja kwenda lingine ili Bunge liweze kulipa madeni kwa wabunge katika kumalizia mwaka wa fedha wa 2016/17.

“Mlipaji Mkuu wa Serikali alipokea maombi ya wabunge na akalazimika kutoa taarifa tu kwa Bunge juu ya uhamisho wa fedha hizo, kama ingekuwa fedha hizo zinatoka nje ya bajeti kuu ndipo angelazimika kupeleka bungeni ili wabunge wapitishe,” amesema Dk Kashilillah.

Amesema Bunge halina mamlaka ya kuchukua fedha bila kupitia kwa mlipaji mkuu wa Serikali.

No comments