Breaking News

Freeman Mbowe Ataka Rais Aombewe Kupunguza Ukali wa Maneno

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewaomba Watanzania wamuombee Rais John Magufuli kwa Mungu ili apunguze ukali wa maneno yake kwani analigawa na kulitia hofu Taifa.

Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni alitoa kauli hiyo juzi na kuirudia jana wakati akihutubia mikutano ya hadhara maeneo ya Masama, Mailisita na Bomang’ombe.

“Nimeongea Bomang’ombe nikampelekea Rais salamu na wasaidizi wake wakanipigia wakaniambia tunakusikia Mbowe... Tumia ulimi laini. Acha ulimi wa maneno makali makali tu kila siku,” alisema. “Mwanadamu saa nyingine wanahitaji wapewe mapenzi ya viongozi. Sio kila siku kiongozi umekaza tu misuli. Kuna mahali unatakiwa uwaambie maneno ya kuwatia faraja.

“Unajenga Taifa lenye upendo sio kujenga Taifa la kutishana tu kila saa. Namuomba Rais aelewe unapokuwa Rais, unakuwa mfariji mkuu. Kauli zako zinaweza kulijenga Taifa au kuliogofya Taifa.

“Rais wetu tumuombee Mungu ampe uungwana wa kujua kuwa anaowaongoza ni binadamu wenye damu wenye nyama, walio maskini na tajiri. Kauli za mkuu wetu wa nchi zinatukwaza.

“Yapo mambo mazuri anayofanya lakini yapo mambo mengine anayofanya na kauli ambazo haziashirii kuwa kiongozi mkuu wa Taifa ni mfariji. Wewe Rais wa nchi, sawa lakini ruhusu tukukosoe.

“Sisi tunaamini huwezi kwenda kwenye wahanga (waathirika)  wa tetemeko la ardhi Bukoba, ukawasimanga badala ya kuwapelekea chakula. Huwezi kutoa kauli kuwa wasio na chakula Serikali haigawi chakula wafe.”

“Hizo sio kauli. Tumuombe Mungu amjaze neema amlegeze ulimi. Ulimi unakaza sana nafikiri mnanielewa.”

Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa muungano wa vyama vinne vya upinzani chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) alisema yako mambo mabaya yanayofanyika katika nchi ambayo alisema wataendelea kuyasema bila ya kuogopa.

“Kwenye nchi zilizoendelea na zinazoheshimu demokrasia, wanaona upinzani kama nyenzo muhimu ya kujenga mshikamano na nguvu ya pamoja ya Taifa. Kwa Serikali yetu ya CCM wapinzani ni maadui.

“Kwa mataifa makubwa yaliyoendelea kama Marekani, Uingereza na Ujerumani, wana vyama vingi vya siasa. Ukienda Marekani wana mtu anaitwa (Donald) Trump na Democrat wana (Hilary) Clinton.

“Wamepambana kwenye uchaguzi na uchaguzi umemalizika hakuna anayempiga mwenzie ngumi. Hapa uchaguzi umeisha miaka miwili lakini bado ni visasi tu. Kamata viongozi, wabunge weka ndani.”

Tangu Rais Magufuli apige marufuku mikutano ya vyama vya siasa na maandamano hadi mwaka 2020, viongozi wa upinzani wakiwamo wabunge, wamejikuta katika msuguano na Jeshi la Polisi.

Ingawa Rais aliruhusu wabunge na madiwani kufanya mikutano katika maeneo yao ya uchaguzi, lakini bado baadhi ya viongozi hao wamejikuta matatani wanapofanya mikutano baadhi wakidaiwa kutoa maneno ya uchochezi au kutopata kibali.

Mbowe yupo katika ziara ya siku nane jimboni mwake, ambako pamoja na mambo mengine, atatembelea miradi ya maendeleo na kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wananchi.

Akizungumza jana katika moja ya mikutano hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Grace Kiwelu alisema Mbowe ameandaa mpango kabambe wa kuwakomboa wananchi wa jimbo hilo kiuchumi.

Kiwelu ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Mkoa wa Kilimanjaro aliwaomba wanawake wa jimbo hilo kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika na mpango huo wa Mbowe.

Ingawa hakufafanua mpango huo utakuwaje, lakini Kiwelu alisema wanawake katika vikundi hivyo watapatiwa fedha za kuanzisha shughuli za kiuchumi ili kujikomboa dhidi ya umaskini.

No comments