BAADA YA KUNUNUA NDEGE SASA GWAJIMA AJA NA HII KALI NYINGINE
Ukiachana na lile dege aina ya Jet lenye thamani ya Sh. Bilioni 2.6 kuzua gumzo, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kwa sasa ameonekana kuwa tishio baada ya kununua ‘madege’ mengine mawili na mtambo wa kufua umeme, Amani linakupa full stori.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Gwajima alitupia mtandaoni ndege aina ya Gulfstream N60983 ambayo aliweka bayana kuwa ameinunua na kuahidi kuishusha Bongo kwa ajili ya matumizi ya kikanisa.
HABARI MPYA SASA
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka kanisani kwa Gwajima, licha ya dege hilo kuzua sintofahamu mitandaoni, waumini wake hawakushtuka kwa sababu walishatangaziwa kuwa kuna madege mengine yatatua muda wowote kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa wanaohitaji wokovu.
“Sisi kama waumini hatuna shaka na Baba Askofu kwa sababu hiyo ndege ambayo ninyi mnaiona dili siyo ishu kubwa kabisa kwani kuna madege mengine mawili yanakuja.
KUMBE GWAJIMA ALISHATANGAZA
“Tangu Januari, mwaka huu, Baba Askofu alishatangaza kuwa ukiachana na ile ndege ndogo, helkopta na hiyo Jet, kuna ndege nyingine mbili zinatakiwa kutua nchini kusaidia huduma ya Mungu.
ZINAFANYIWA MCHAKATO
Kutokana maelezo hayo, Amani lilimtafuta Askofu Gwajima ili kuzungumza naye lakini ikashindikana na kupata nafasi ya kuzungumza na Afisa Habari wa Kanisa la Uzima na Ufufuo, David Mgongolwa ambaye alikiri kuwepo kwa ndege hizo, lakini kuhusu sintofahamu iliyotokea alisema suala hilo hana mamlaka nalo zaidi.
“Kuhusu suala la Jet kuzua gumzo mimi sina mamlaka nalo, hilo atajibu askofu akirudi nchini hivi karibuni. Hii Jet ni ndege ya tano Bishop analeta nchini. So anajua anachofanya. Akirudi ataongea.
“Hizi ndege zinafanyiwa mchakato na pindi zikikamilika Bishop mwenyewe atatangaza. Kwani kila kitu kiko wazi hata kanisani alishatangaza kuhusu ujio na ndege hizo.
“Ni suala la muda kwani hata helkopta ilifika muda mrefu, lakini ilikuja kuzinduliwa baada ya mwaka mmoja kwa hiyo hata hizo nyingine usiwe na haraka, utasikia tu,” alisema Mgongolwa.
KWELI GWAJIMA NI TISHIO
Gwajima anaonekana ndiye anayeongoza wachungaji wenzake kwa kuwa na mali nyingi anazomiliki.
Mbali na helkopta na hiyo Jet mpya, anatajwa kuwa na ndege nyingine huku nyingine mbili zikiwa njiani kuja na kukamilisha idadi ya ndege tano.
ALETA MTAMBO WA KUFUA UMEME
Ukiachana na hayo madege ambayo amewahi kuyataja kanisani kwake kama waumini na msemaji wake walivyosema, Gwajima ameeleza kupitia mtandao kuwa atashirikiana na Wajerumani kuleta mtambo wa kufua umeme wa Megawati 250 unaotajwa kugharimu mamilioni.
“Namshukuru Mungu nimepata umeme Megawati 250 niliopewa na rafiki zangu Wajerumani na nilimtuma Engineer Mkuu wa Ufufuo na Uzima Duniani Eng. Yeconia Bihagaze kwa ajili ya kufuatilia,” aliandika Gwajima.
AHADI YA TRENI
Huko nyuma, Gwajima alishawahi kuahidi kuleta treni ya umeme ya kisasa ambayo itafanya safari yake Dar hadi Morogoro ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano yenye Kaulimbiu za ‘Hapa Kazi Tu’ na ‘Tanzania ya Viwanda’.
MAGARI NAYO
Kwa upande wa magari, Gwajima anatajwa kumiliki magari mengi ya kifahari likiwemo gari la kifahari aina ya Hummer 2 ambalo gharama ya manunuzi mpaka kufika Tanzania ni wastani wa shilingi milioni 250.
MAGARI YA WACHUNGAJI
Baadhi ya wachungaji wake wanamiliki magari aina ya Subaru Forester (sokoni linauzwa shilingi milioni 17), Mitsubishi Pajero (shilingi milioni 16), Toyota Spacio New Model (shilingi milioni 20), Toyota Harrier Lexus (shilingi milioni 35) na Toyota Land Cruiser V8.
MIKUTANO YA NJE YA NCHI
Gwajima pia amekuwa akiingiza mamilioni ya pesa kutokana na safari za Ulaya na Marekani ambako kila ifikapo mwezi Juni wa kila mwaka huenda kufundisha neno la Mungu na hulipwa si chini ya dola 2000 kwa siku (zaidi ya shilingi milioni 4 kwa siku.)
IDADI YA WAUMINI WENGI
Ukiachana na vitu vyote, Gwajima ni miongioni mwa wachungaji wenye idadi kubwa ya waumini nchini ambapo waumini wake wanakadiriwa kufika elfu sabini huku idadi yake ya makanisa zaidi ya mia tatu duniani yakiwa chanzo cha yeye kutisha kwa ukwasi.
MWANDISHI WA VITABU
Hata hivyo, Gwajima amekuwa akitumia fursa ya waumini wake alionao kuandika vitabu mbalimbali vya kuwajenga na kuwaimarisha kiroho kisha kuviuza kwa bei mbalimbali. Ambapo zaidi ya vitabu 40 tofautitofauti ameshaviandika hadi sasa huku kitabu kimoja kikiuzwa si chini ya shilingi elfu kumi.
MJENGO WA GHOROFA NNE
Ukiachana na nyumba ambazo hazifahamiki, anamiliki mjego wa ghorofa nne uliopo Salasala jijini Dar.
No comments