Raila Odinga ampaisha Magufuli Afrika
MGOMBEA Urais nchini Kenya kupitia muungano wa vyama vya ODM, ANC, WIPER , Chama Cha Mashinani (CCM) na Ford Kenya (NASA), Raila Odinga amemmwagia sifa Rais John Magufuli kwa uongozi wake thabiti wa kupambana na rushwa, watumishi hewa, ufisadi na kutetea na kulinda rasilimali za taifa.
Amekwenda mbali zaidi na kusema Rais Magufuli ni mfano wa kuigwa barani Afrika. Raila alitoa pongezi hizo wakati wa mkutano wake wa kampeni katika mji wa Isebania katika Kaunti ya Migori, iliyopo mpakani mwa Kenya na Tanzania, upande wa Sirari, Tarime mkoani Mara.
Aliwaomba wananchi kumpa kura na wagombea wa NASA madiwani, magavana na wabunge ili aweze kuondoa ufisadi nchini mwao.
Akiwa katika Stendi ya magari ya mjini Isebania ambako alitua kwa helikopta yake akiongozana na baadhi ya viongozi wa muungano wa vyama vinavyounda NASA akiwemo Moses Wetangula, Gavana wa Migori anayetetea nafasi hiyo Zakaria Obado, mgombea ubunge Jimbo la Kurya West, Matiko Bhohoko, Jane Moronge, mgombea ubunge Kurya East, wagombea udiwani maeneo ya Bukira West John Tobocho, Nelson Bajah, Elias Nyahure na Kiongozi wa NASA Kurya West Peter Masaithe kwa jina maarufu Highyway na kulakiwa na maelfu ya wakazi wa mji huo wa Isebania na vitongoji vyake.
Huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu, Raila aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya, alisema; “Uongozi wa Rais John Magufuli ni mfano wa kuigwa na viongozi wengine wa Afrika ambao ni wazalendo na nchi zao, wanaotetea wananchi wao hususani wanyonge ambao ndio wengi, wanaopambana na ufisadi kutoka moyoni mwao na mafanikio kuonekana.
“Nikifanikiwa kuwa rais nitafuata nyao zake nitamuomba anipe ufagio wa mafisadi niwafagie hapa Kenya, hapa kwetu wananchi wamekuwa masikini, hakuna chakula, sukari na vitendo vya ufisadi viko juu wananchi wanafananishwa na punda aliyebeba mzigo mkubwa ambao hauwezi… lazima huu mzigo tuuteme na kuwapumzisha wananchi wetu.
“Mkinichagua, wanafunzi watasoma bure hadi kidato cha nne, miundombinu itatengenezwa, barabara za lami kwani mimi ni mhandisi wakati nikiwa Waziri wa Ujenzi hizi barabara mnazotumia nilizilima mimi na tangu hapo hakuna kilichoendelea hazikukarabatiwa kutokana na ufisadi uliokithiri.”
Mgombea Ugavana wa Migori, Obado alisema; “Nimekuwa gavana wa Kaunti ya Migori nafikiri wakazi wa kaunti hii mnafahamu juhudi zangu nilizofanya kwa kuwaletea maendeleo bila ubaguzi wowote ninawaomba mnipe kura na urais mpeni mgombea wetu wa NASA Raila Odinga, huyu ndiye kiongozi shujaa wa kuweza kupambana na ufisadi hapa nchini nasi tutakuwa nyuma yake kupambana na wanyakuzi wa mali ya wananchi.”
No comments