Breaking News

Ndugu wa Kamusoko kutua Dar

Kocha mkuu, George Lwandamina.

MIDO mpya anayewaniwa na Yanga, Mcongo, Papy Kabamba Tshishimbi ‘Rasta’ ameshindwa kutua kwa wakati ndani ya kikosi hicho, baada ya kocha mkuu, George Lwandamina kuahirisha usajili wake huku akielekeza jina la kiungo mmoja kutoka nchini Zimbabwe, kuwa ndiye asajiliwe. 

Tshishimbi anayeichezea Mbabane Swallows ya Swaziland, alitakiwa kutua Jumapili ya wiki iliyopita kwa ajili ya kumalizana na Yanga lakini kwa sasa dili lake limewekwa pembeni baada ya Lwandamina kupendekeza kusajiliwa kwa kiungo mwingine. 

Chanzo kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Championi Jumatano kuwa, usajili wa Tshishimbi kwa sasa umesimamishwa baada ya Lwandamina aliyefika nchini juzi, kuwadokeza viongozi wafanye haraka kwenda kumsaini kiungo wa timu ya taifa ya Zimbabwe nchi anayotoka kiungo wao Thabani Kamusoko ambayo imeshiriki michuano ya Cosafa inayofanyika Afrika Kusini. 

“Kocha baada ya kurudi kutoka Afrika Kusini, ameamua kusimamisha kwanza tusimsajili Tshishimbi kwa sababu kuna kiungo mmoja kutoka Zimbabwe ambaye amemuona anafaa zaidi kuliko yeye, hivyo ametupa agizo la kuhakikisha tunamnasa haraka iwezekanavyo. 

“Lakini kama tutashindwana naye katika suala la maslahi, kocha ameelekeza turudishe mawazo kwa Tshishimbi kwani kwa sasa amemuweka chaguo la pili japo tutampata kiurahisi kwani dau lake ni dogo tofauti na kiungo huyo,” kilisema chanzo hicho. Hata hivyo, baadhi ya taarifa zinasema Yanga imeamua kuweka kiporo Tshishimbi baada ya kusikia Simba nao wanamfukuzia. Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniphace Mkwasa, aligoma kuzungumzia ishu hiyo, hata baada ya kutafutwa mara kadhaa.

No comments