Breaking News

Mvutano mkali wabunge, wadau sheria ya madini

Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, akizungumza wakati wa utoaji wa maoni ya wadau kuhusu miswada ya Hati ya Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika mikataba ya Maliasili za Nchi mwaka 2017, bungeni Dodoma jana. Picha na Emmanuel Hermani

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa (CCM) aliahirisha kikao hicho wakati moto ukiwaka na wadau wakizidi kung’ang’ania muda wa kujadili miswada inayoweka mwongozo wa umiliki na usimamizi wa mikataba ya madini uongozwe na pia iandikwe kwa lugha ya Kiswahili

Dodoma. Kikao cha Kamati ya Katiba na Sheria kwa ajili ya kusikiliza maoni kuhusu miswada ya marekebisho ya sheria kuhusu maliasili za nchi, jana kiliisha kwa mzozo baina ya wabunge na wadau waliojiegemeza kwenye muda mfupi na lugha iliyotumika.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa (CCM) aliahirisha kikao hicho wakati moto ukiwaka na wadau wakizidi kung’ang’ania muda wa kujadili miswada inayoweka mwongozo wa umiliki na usimamizi wa mikataba ya madini uongozwe na pia iandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

Ilifikia wakati katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilila alimtaka mwenyekiti wa kamati hiyo achuje wadau wenye hoja zinazozungumzia vifungu vya sheria hizo ndio waruhusiwe kuzungumza na kuachana na waliokuwa wanataka muda wa kujadili uongezwe na lugha ya miswada hiyo iwe Kiswahili.

Wadau hao walikuwa wakitoa maoni yao kuhusu miswada hiyo na baadaye wabunge kupewa nafasi ya kuuliza maswali matatu, lakini hoja za wageni hao zikaonekana kuudhi watunga sheria.

Akijibu hoja za wadau hao, mbunge wa Newala Mjini (CCM), George Mkuchika alisema muswada huo umefuata kanuni zote zinazotakiwa kufuatwa na Spika pamoja na wabunge wameridhia kuujadili kwa ajili ya hatua zaidi.

Wakati akizungumza, mmoja wa wabunge wa kambi ya upinzani bungeni alidakia na kusema “babu usidharau wapiga kura wako”.

Baadaye, mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Jaffar Michael alisimama na kutaka wadau hao waachiwe kutoa maoni yao bila kuingiliwa kwa sababu wabunge wana nafasi yao.

Na walipopata nafasi waliendelea kusisitizia suala la muda na lugha.

Hatua hiyo, ilimfanya Kashililah kutaka wadau wajielekeze kwanza katika muswada kwa kutaja vifungu wanavyotaka kutoa maoni yao.

“Wote ambao mimi niliwaalika niliwapa nakala ya miswada yote, hivyo anayekuja hapa ajielekeze katika kifungu anachotaka kutoa maoni yake,” alisema.

Hata hivyo, mwongozo huo haukupokelewa vizuri na wadau, hivyo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kulazimika kutoa ufafanuzi.

Lukuvi alisema baadhi ya wadau walikuwa wakipoteza muda kwa kuongea mambo yasiyo katika muswada huo.

“Bahati nzuri tunao watu wa sektarieti wengi tu wanaweza kuwachuja hao kabla ya kuja katika ukumbi ili kufahamu ni nani hasa mwenye maoni,” alisema.

Akiahirisha mkutano huo, mwenyekiti wa kamati hiyo alisema wanaongozwa na kanuni na kwamba hawabani idadi ya wadau wanaowasikiliza.

“Nataka niwaambie kuwa tunafanya makosa makubwa sana ambayo tutakuja kujuti. Huu ndio wakati ambao Bunge linatunga sheria na wala si ndani ya bunge lakini haya tunayoyaona hapa nawaambia ukweli tutakuja kujuta,” alisema Mcherwa’

“Makelele mnayopiga hayaingii mahali popote kwenye hanrsad (kumbukumbu rasmi za Bunge), hayaingii wala sisi kama kamati hakuna tunalolichukua. Tunachukua point inayotusaidia na wale ambao wametumwa, hawatusaidii.”.

Mwenyekiti wa kamati ya Nishati na Madini, Dotto Biteko alisema haiwezekani wadau wanaotoka katika taasisi sita wote wawe na maoni yanayofanana kuanzia mwanzo hadi mwisho.

“Hili jambo linatupa mashaka na linatuonyesha kuwa hatuna nia njema na sheria hii. Hatua tuliyofika hatuwezi kurudi nyuma tunakwenda mbele lazima ifike mwisho,” alisema.

Juzi wakati wa kujadili miswada hiyo, wabunge wengi walionyesha hofu yao katika mambo manne ambayo ni usalama wa madini yatakayohifadhiwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kabla ya kuuzwa, uwezo wa bima za hapa nchini, kutumia uzoefu wa nchi nyingine na ushiriki wa Serikali katika shughuli zote za uchimbaji.

Pia, wabunge walitaka kujua jinsi wakazi wanaozunguka migodi watakavyonufaika na maliasili hizo.

Wakizungumza wakati wa kujadili muswada huo uliowasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, wabunge wengi walihoji mambo hayo na kutaka Serikali ifanyie kazi.

“Sijui tunaweka insurance (bima) gani? Sio watu wameweka capital (mitaji) yao, halafu wewe unachukua unaenda kutunza. Sijui hili mmeliangaliaje? Watanzania wasije kupata matatizo bure,” alisema mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche.

Heche alikumbusha tukio la mwaka 1984 wakati BoT ilipoungua, akitaka Serikali iangalie suala hilo ili Watanzania wasije kuingia tena kwenye matatizo.

Mwingine aliyehoji ni mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Rashid Akibar aliyesema awali BoT iliwahi kutunza dhahabu, lakini baada ya muda walikuta mchanga na si dhahabu tena.

“Naomba mheshimiwa waziri utuweke sawa hapo ili tusikute mchanga tena,” alisema.

Alisema dhahabu ni rahisi sana kuchukuliwa kuliko fedha na kuhoji Serikali iko tayari kuchukua ulinzi nchini Marekani kwa ajili ya kuboresha.

Wasiwasi kama huo alikuwa nao mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almasi Maige ambaye alisema zamani BoT walikuwa wananunua na kuhifadhi dhahabu lakini kuna wakati baada ya miaka mitano iliyeyuka na kushauri eneo hilo kuangaliwa.

“Utaalamu wa BoT ni utunzaji wa fedha si utunzaji wa dhahabu. Hata katika nchi 100 ambazo zinahifadhi dhahabu, Tanzania haipo,” alisema.

Naye mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi alisema iwapo muswada huo utapitishwa, utaunda chombo cha kusimamia madini na kushauri kiwe na vitendea kazi kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Mmeweza kujifunza kutoka nchi kama Ghana?” alihoji.

Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda alisema muswada huo uweke wazi juu ya kufutwa kwa baadhi ya miundo katika Wizara ya Nishati na Madini.

Alisema kwa jinsi muswada huo ulivyo unahamishia shughuli zote za kamishna wa madini kwa ofisa mtendaji mkuu wa kamisheni itakayoundwa.

Akijibu hoja hizo, Profesa Florence Luoga wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) aliwaondoa hofu wabunge katika suala la bima, akisema utekelezaji wake hauhitaji kuwa na kampuni za bima za kimataifa kwa kuwa uwekezaji unafanyika nchini.

“Risky (janga) ni ya ndani. Tunaposema watalazimika kuweka bima ina maana ni kampuni za wazawa,” alisema Profesa Luoga.

Kuhusu kampuni za madini kulazimishwa na sheria kuwa na akaunti nchini, Luoga alisema hiyo ni hoja ya kukuza uchumi.

“Hii itaongeza uwezo wa benki zetu. Hawa wana haki na gawio lao tu wanaweza kuweka katika akaunti za nje ya nchi,” alisema.

Aliwataka wabunge na Watanzania kutowafurahisha wawekezaji hadi wakajidhulumu.

Kwa upande wake Profesa Kabudi aliwaondoa hofu wabunge kuhusu usalama wa BoT kwa sababu wakati inaungua ilikuwa na mbao nyingi.

Hata hivyo, alisema kuwa teknolojia imekua na jengo hilo limewekwa vifaa vya utambuzi wa moto.

Pia, alisema ripoti za makinikia haziwezi kuletwa bungeni kwa sababu ni mali ya Rais John Magufuli na kwamba labda mwenyewe atake kufanya hivyo.

Alisema wameangalia uzoefu wa nchi mbalimbali kama Botswana, Sierra Leone, Indonesia, Saudi Arabia na Ghana.

Gerald Mturi, katibu mtendaji wa Chama cha Nishati na Madini ((TCEM) kinachowakilisha wachimbaji wakubwa, alisema kupeleka shauri mahakama za kimataifa kunaongeza kujiamini kwa uwekezaji.

“Naomba kipengele kinachotaka mahakama za ndani kusikiliza migogoro hii, kiondolewe,” alisema.

Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Mawakili Watetezi wa Mazingira (Leat), Dk Rugemeleza Nshala alisema kama kutakuwa na mgogoro wowote unaopitiliza uwezo wa mahakama za ndani, sheria itambue kuwa ni batili.

“Kama wataalamu wetu hawana uwezo wa kusikiliza migogoro hiyo basi wapelekwe shule kuwajengea uwezo huo, lakini kesi hizo zisikilizwe nchini,” alisema Dk Nshala.

No comments