Manji , wenzake wataka wafunguliwe mashtaka
Wakili asema mteja wake huyo yuko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anakopatiwa matibabu akiwa chini ya ulinzi
Mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji na wenzake wawili wamewasilisha maombi Mahakama Kuu wakiiomba iliamuru Jeshi la Polisi liwafungulie mashtaka mahakamani au liwaachie huru.
Manji na wenzake Deogratius Kisinda na Thobias Fwere, waliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo jana kupitia kwa Wakili Hudson Ndusyepo, baada ya kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, tangu Jumamosi.
Pia, Manji alikumbwa na msukosuko mwingine baada ya watu waliodaiwa kuwa ni wafanyakazi wake kukamatwa na Uhamiaji kwa kuishi nchini kinyume cha sheria wakati si raia na sasa ni hili la kudaiwa kukutwa na nguo za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Hata hivyo, Wakili Ndusyepo amesema jana kuwa mteja wake huyo yuko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anakopatiwa matibabu akiwa chini ya ulinzi.
Jana, wakili huyo alifungua maombi mahakamani hapo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam, (ZCO).
Katika hati ya kiapo kinachounga mkono maombi hayo, Wakili Ndusyepo anaeleza kuwa walalamikaji walikamatwa na kushikiliwa na ZCO kwa nyakati tofauti.
Hati hiyo inaeleza kuwa Kisinda alikamatwa Juni 30 saa 10 jioni wakati Manji na Fwere walikamatwa Julai Mosi na saa tano asubuhi, katika jengo la Quality Centre na kwamba wameendelea kushikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi hadi sasa.
Katika mahojiano na gazeti hili jana, Naibu Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Lucas Mkondya ameeleza kuwa Manji anashikiliwa tangu Jumamosi ya wiki iliyopita kwa ajili ya mahojiano kuhusu kukutwa majora 43 ya sare za JWTZ na mihuri 39 ya kampuni tofauti na baadhi ya kambi za jeshi.
“Tulipata taarifa kutoka kwa wasiri wetu kwamba katika godauni lililopo katika ofisi zake Chang’ombe anahifadhi sare za JWTZ. Tarehe moja mwezi huu tulikwenda kufanya upekuzi wa ghafla ndipo tutakuta majora 35 na kesho yake tukakuta mengine manane na hiyo mihuri,” amesema Mkondya.
No comments