Kinga ya Ukimwi Yaanza Kuonyesha Mafanikio
Utafiti wa kinga ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi, ulioanza kufanywa nchini miaka kadhaa iliyopita umeana kuonyesha mafanikio.
Lakini watafiti wamesema Watanzania watahitaji kuwa uvumilivu wa miaka michache ijayo kusubiri hatua za mwisho za ukamilishaji utafiti wa kinga hiyo kabla haijaanza kutimika rasmi.
Taarifa hizo zinakuja ikiwa wiki moja baada ya Kenya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuanza kutumia dawa ya ugonjwa wa Ukimwi ambayo inaweza kuboresha afya na kurefusha maisha ya maelfu ya watu ambao wanasumbuliwa na magonjwa nyemelezi na ambayo hayakubali tiba nyingine.
Kwa miaka kadhaa Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS) imekuwa ikiendesha utafiti kuhusiana na chanjo ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi na katika hatua ya awali utafiti huo uliwahusisha baadhi ya watu wanaishi na virusi hivyo.
Akizungumzia hatua zilizofikiwa tangu kuanzishwa kwa utafiti huo, mkurugenzi wa mafunzo endelevu na weledi wa MUHAS, Dk Doreen Mloka amesema ingawa bado ni mapema kubainisha utafiti huo lakini kwa ujumla wake umeanza kuzaa matunda.
Amesema matokeo ya awali yanaonyesha kuwa watu waliopatiwa chanjo hiyo wamekuwa na maendeleo mema kwa afya zao kuimarika maradufu tofauti na wale wanaotumia dawa nyingine za kawaida.
Amesema kutokana na matokeo hayo wataalamu wanaofanyia uchunguzi chanjo hiyo sasa wanatengeneza mkakati maalumu ambao unaweza kuchukua muda wa miaka mitano hadi sita kabla ya chanjo hiyo kuanza kutumika rasmi.
“Tumepiga hatua kubwa katika utafiti huu kwa vile tumeona kuwa wagonjwa waliopewa kinga hii afya zao zimeimarika na kiwango cha kinga mwili kinapanda lakini siyo kwa kiwango tulichotarajia lakini kuna utofauti na walivyokuwa wakitumia chanjo za awali,” amesema.
Mtaalamu huyo ameeleza kuwa baadhi ya dawa zinazotumika sasa zimebainika kuwa na hali ya usugu kutibu magonjwa nyemelezi hivyo watafiti wanaendelea kukuna vichwa vyao kusaka majibu yatakayosaidia kupendekezwa kwa dawa mbadala.
Wiki iliyopita Serikali ya Kenya ilitangaza kuanza kutumia dawa mpya inayotambulika kwa jina la Dolutegravir (DGT) ambayo inatajwa kuwa ni chaguo la kwanza kwa watu wanaishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) katika nchi za watu wenye kipato kikubwa kwa kuwa zina athari chache kuliko dawa za ARV zinazotumiwa sasa( yaani kidonge kimoja kidogo kila siku).
Mwaka 2015 Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilipendekeza DGT iwe chaguo la kwanza watu wazima na vijana, lakini hadi katika siku za hivi karibuni watu wanaoishi na VVU katika nchi kama Kenya walikuwa hawezi kupata dawa hizo.
Kuhusu kutumika kwa dawa kama hiyo nchini, Dk Mloka alisema inaweza kutumika lakini bado wataalamu wanaendelea na utafiti kubaini kiwango cha usugu kwa dawa zinazotumika sasa kutibu magonjwa nyemelezi.
“Tunaendelea na utafiti ili kujiridhisha kwamba sisi tupo sawa na Kenya tuingize dawa mpya ama tuendelee na zile za zamani kwa sababu kuleta dawa mpya ni gharama sana,” amesema.
No comments