Hatma ya Uchguzi TFF kujulikana leo
HATIMA ya kuendelea kwa mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao unatarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu, itajulikana leo baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kumalizika.
Kikao hicho kitakachofanyika leo jijini Dar es Salaam, ni kutokana na ombi lililowasilishwa Jumamosi iliyopita na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Revocatus Kuuli kufuatia kugawanyika kwa kamati hiyo.
Kuuli aliwasilisha ombi hilo kwa Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi, ambaye aliridhia kuitisha kikao hicho ili kuamua hatima ya uchaguzi huo ambao utawaweka viongozi wapya madarakani kwa muda wa miaka minne ijayo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji wa TFF, Alfred Lucas, alisema kikao hicho kiko kama ilivyotangazwa na maandalizi yake yamekamilika.
"Ni kikao cha dharura kama ambavyo Kaimu Katibu Mkuu Salum Madadi alivyosema, wajumbe wote wameshajulishwa kuhusu kikao hicho, tusubiri tusikie uamuzi utakaotolewa," alisema kiongozi huyo.
Habari za ndani ambazo gazeti hili imezipata jana zinaeleza kuwa Kamati ya Uchaguzi itavunjwa, lakini Kuuli ataendelea kuwa mwenyekiti huku wajumbe wengine wapya wakiteuliwa kujaza nafasi za ambao wameondolewa.
"Na suala la mahali ambako mkutano mkuu utafanyika pia linaweza kujadiliwa kwa sababu uamuzi wa kuupeleka uchaguzi Dodoma ulifanywa na Malinzi (Jamal) peke yake na halikupewa baraka na Kamati ya Utendaji," kilisema chanzo chetu.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa wajumbe wengi wa kikao hicho wamejiandaa kupendekeza tarehe hiyo hiyo ya uchaguzi iendelee na wao malengo yao ni kuhakikisha wanaboresha upungufu na changamoto ambazo zimebainika tangu kuanza kwa mchakato huo wa uchaguzi.
"Yote haya yanafanyika kwa maslahi ya mpira wetu, pia tusubiri na ujumbe wa Fifa utakavyokuja utakuwa na salamu gani," alisema mjumbe mwingine mwenye nguvu katika kamati hiyo ya utendaji.
Kuuli alilazimika kusitisha mchakato wa uchaguzi baada ya yeye na wajumbe wenzake kutofautiana katika kuamua kukata majina ya wagombea huku pia akikataa kumjumuisha Malinzi kwa sababu hawakumfanyia usaili ana kwa ana.
No comments