Breaking News

FAIDA ZA PARACHICHI

Parachichi ni tunda ambalo mti wake hujulikana kisayansi kama Persea amerikana . Tunda hili lina aminika kuwa na asili kutoka jimbo la Puebla, bara Amerika ya kusini kunako nchi ya Mexico. Ushahidi wa kale kabisa, takribani miaka 10000 BC umeonyesha parachichi lilitumika katika jimbo la Puebla nchini Mexico. Lakini kutokana na faida nyingi kiafya zipatikanazo kwa ulaji wa tunda hili, tunda hili sasa hupatikana na kutumika kwa lishe sehemu nyingi duniani hususani barani Afrika.

Parachichi ni tunda la pekee ukilinganisha na matunda mengine, kimsingi matunda mengine huwa yana wanga( carbohydrate ) kwa wingi, wakati parachichi lina aina ya mafuta ambayo yana faida kwa afya.
Jedwali likionyesha kiasi cha virutubisho katika gramu 100 za
parachichi.
Aina ya kirutubisho Kirutubisho Kiwango kilichopo
Vitamini Vitamini A 7ug
Vitamini E 2.1ug
Vitamini C 10mg
Thiamine 0.1mg
Niacini 1.7mg
Vitamini B 6 0.3mg
Folic acid 81ug
Madini Kalshamu 12mg
Phosphorasi 52mg
Magnesiamu 29mg
Potasiamu 599mg
Munyu (Sodium) 7mg
Chuma 0.6mg
Zinki 0.6mg
Shaba 0.2mg
Manganizi 0.1mg
Protini muhimu TRP(Tryptophan) 25mg
THR(Threonine) 73mg
ILE(Isoleucine) 84mg
LEU(Leucine) 143mg
LYS(Lysine) 132mg
MET(Methionine) 30mg
CYS(Cysteine) 27mg
PHE(Phenylalanine) 232mg
TYR(Tyrosine) 49mg
VAL(Valine) 107mg
ARG(Arginine) 88mg
HIS(Histidine) 49mg
Parachichi katika tafiti nyingi limeonekana kuwa na faida katika afya ya moyo. Wagonjwa wa moyo wamekuwa katika makatazo ya kutumia aina ya mafuta ambayo yamekuwa yakichangia kuongezeka kwa lehemu katika damu(mafuta hayo kitaalam kama
polysaturated fat ), na kuongeza matumizi ya mafuta yasiyoongeza lehemu katika damu ( monosaturated fat ). Parachichi ni chanzo kizuri cha mafuta yasiyoongeza lehemu katika damu. Utafiti unaonyesha kuwa matumizi ya mafuta haya katika parachi hupunguza lehemu iliyo hatari ( kitaalam kama, Low density lipoprotein ), na huchangia katika ongezeko la lehemu isiyo hatari( High density lipoprotein ).
Madini ya Potasiamu ni aina ambayo huwa watu hawapati ya kutosha kutoka katika vyakula. Parachichi lina kiwango kikubwa cha madini ya potassium kuliko ndizi. Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa matumizi ya madini haya huambatana na kupungua kwa shinikizo la damu, shinikizo la juu la damu laweza kupelekea mtu kupata kiharusi, shambulizi la moyo hata figo kushindwa kufanya kazi.
Parachichi lina kiwango kikubwa cha fiba. Fiba ni kirutubisho kutoka katika vyakula vya jamii ya mimea, fiba huwa hazimeng’enywi tumboni lakini huwa zina umuhimu mkubwa sana, kama kusaidia kupunguza uzito wa mwili, kusaidia urekebishaji wa kiwango cha sukari mwilini na kupunguza hatari ya kupata magonjwa mengi mwilini. Kuna aina fulani ya fiba ambazo huwa ni virutubisho kwa ajili ya bakteria wenye faida tumboni, hii huimarisha kinga ya mwili na kusaidia mwili kufanya kazi katika kiwango kinachotakiwa. Kwa kuwa parachichi lina kiwango kikubwa cha fiba, husaidia kuboresha mmeng’enyo na kupata choo katika hali ya kawaida.
Aina ya mafuta na virutubisho tulivyoviona awali katika parachichi vinasaidia afya ya ngozi yako. Husaidia ngozi yako kutokuwa kavu na kuwa na unyevu unaotakiwa na kuifanya ngozi kuwa laini na yenye afya. Vitamini C husaidia katika kusaidia uponaji haraka wa ngozi na kujijenga upya kwa seli za ngozi zilizoharibika,husaidia kujenga
elastini na collageni ambazo ni muhimu katika ngozi. Uwepo wa virutubisho viondoavyo sumu( antioxidants ) katika parachichi kama carotenoidi na vitamini E, hutusaidia kutukinga na mionzi mikali ya jua, kwa hiyo huzuia makunyanzi katika ngozi na kuifanya ngozi yako kuwa na mwonekano mzuri wakati wote.
Tunda hili ni lishe bora kwa wale wenye kisukari. Parachichi lina kiwango kidogo cha sukari ukilinganisha na matunda mengine. Pia uwepo wa mafuta aina ya ‘ monosaturated’ husaidia kuboresha ufanyaji kazi wa homoni ya insulini, katika urekebishaji wa kiwango cha sukari mwilini. Faida nyingine ni kuwa Vitamini C katika parachichi husaidia kuimarisha mishipa ya damu na kuboresha kinga ya mwili ambayo ni faida kubwa kwa wagonjwa wenye kisukari.
Faida katika afya ya uzazi ni dhahiri. Parachichi lina Vitamini E ambayo ni “ antioxidant ” Potasiamu, Vitamini B6,Vitamini C ambazo hutusaidia kutukinga na magonjwa ya moyo hata yale ya kisukari. Chochote kile kinachosaidia afya ya moyo pia husaidia afya ya uzazi. Wanaume wenye magonjwa ya moyo na kisukari huwa tatizo kubwa la upungufu wa nguvu za kiume.
Parachichi pia limeonekana kuwa na faida nyingi katika kuboresha afya ya macho, viungo vya mwili na nyinginezo nyingi. Katika utafiti mmoja uko Marekani, ulionyesha kuwa watu walao parachichi walionekana kuwa na afya bora ukilinganisha na wale wasiokula parachichi. Waliokula parachichi hawakupatwa na matatizo ya
mmeng’enyo ukilinganisha na wale wasiokula. Matatizo ya mmeng’enyo huchangia watu kupatwa na magonjwa ya moyo na kisukari.
Unasubiri nini sasa? Anza kutumia matunda haya kuboresha afya yako. Unapokwenda sokoni usisahau kununua parachichi.Faida ni nyingi zitokanazo na ulaji wa tunda hili.


No comments