Serikali yatoa Sababu Zinazowafanya CHADEMA Wapigwe Marufuku Kufanya Sherehe Vyuoni
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alihoji bungeni sababu za wanafunzi wa CCM kupendelewa kufanya mikutano na sherehe za kumaliza masomo yao huku wanafunzi wa vyama vingine vya upinzani hasa CHADEMA kupigwa marufuku kufanya sherehe hizo.
Akijibu jambo hilo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema kuwa wanafunzi wa Chama Cha Mapinduzi huwa wanafuata utaratibu ndiyo maana huwa wanapewa ruksa kufanya sherehe hizo pindi wanapomaliza vyuo na kusema hao wengine huwa hawafuati utaratibu ndiyo maana wanakuwa wanazuiliwa.
"Taratibu ziko wazi kama CCM walikuwa wamefuata utaratibu na kupewa mikutano, chama kingine chochote kinachotakiwa ni kufuata utaratibu zile zile waweze kupewa mikutano lakini wengine kama hawajafanya utaratibu hawatapewa tu kwa sababu CCM walipewa bali watapewa kwa kufuata utaratibu, kuna sehemu zingine CHASO hao hao wamepewa mikutano kwa hiyo linalotakiwa ni utaratibu tu wa kupewa mikutano hiyo" alisema Mwigulu Nchemba
Mbali na hilo Waziri Mwigulu Nchemba alisema mikutano ya hadhara haijazuiwa bali imewekewa utaratibu na kusema duniani kote sifa za mikutano ya hadhara ni kama ambavyo inafanyika hivi sasa Tanzania na kusema kuwa mtu aliyeshinda ndiye anaendelea na majukumu ya kuongoza na aliyeshindwa hapaswi kushukuru kwa wananchi.
"Marekani mwaka jana walifanya uchaguzi mmemuona Hillary Clinton anashukuru kwa wananchi? Duniani kote aliyeshinda ndiye anaendesha serikali kwa utaratibu wa kiserikali hili liko wazi duniani kote" alisisitiza Mwigulu Nchemba
No comments