Breaking News

Sekondari 1696 kunufaika na Bilioni 16.9/-

  Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (mwenye tai nyekundu) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.

  Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (kulia) akikabidhi moja ya kifaa cha kufundishia masomo ya sayansi kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Juhudi wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum  mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.

Serikali imetumia shilingi bilioni 16.9 kununua vifaa vya maabara na vile vya wanafunzi wenye mahitaji maalum vitakavyonufaisha shule za sekondari 1696 ambapo shule 1625 ni za Kata na 71 ni kongwe ambazo kwa sasa zipo katika ukarabati.

Akihutubia wakati wa hafla ya kuzindua  mpango wa  kusambaza vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum leo Jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa inaboresha sekta ya elimu  ili azma ya ujenzi wa Tanzania ya Viwanda itimie kwa kuwa Taifa litaweza kuzalisha wanasayansi kulingana na mahitaji.

“Tunatoa vifaa hivi kwa awamu ya kwanza kwa shule zilizokamilisha ujenzi wa maabara, hivyo ni matumaini yangu kuwa wale ambao hawajakamilisha watafanya hivyo ili awamu ijayo nao wapate vifaa hivi.” Alisisistiza Majaliwa.

Aliongeza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha zaidi ya shule 4,000 nchini zinakuwa na vifaa vya maabara, walimu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia na mazingira rafiki ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora itakayowasaidia kushiriki katika ujenzi wa Taifa.

Pia Waziri Mkuu ameonya kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya mtu yoyote atakaye sababisha mwanafunzi wa kike kupata ujauzito na kushindwa kuendelea na masomo ambapo atakabiliwa na adhabu ya kwenda jela miaka thelathini.

“Awe baba au mama au mtu yoyote ambaye itathibitika kuwa amemsababishia ujauzito mwanafunzi, adahabu yake ni kifungo cha miaka thelathini jela.” Alisisitiza Majaliwa.

  

No comments