Breaking News

KONTENA nyingine zenye malighafi za kutengeneza dawa za kulevya zimekamatwa katika bandari kavu ya AMI iliyoko Tabata relini jijini Dar es Salaam


KONTENA nyingine zenye malighafi za kutengeneza dawa za kulevya zimekamatwa katika bandari kavu ya AMI iliyoko Tabata relini jijini Dar es Salaam.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga, aliiambia Nipashe jana kuwa kontena hizo zilizokamatwa ni mbili, moja ina urefu wa futi 20 na nyingine futi 40, zote mali ya Tecno Net Scientific na zinaweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya cocaine na mandrax.

Alisema makontena hayo yametoka Ufaransa na India kwa meli ya CMA na yaliondolewa kwenye Bandari ya Dar es Salaam wiki tatu zilizopita kabla ya kupelekwa kwenye bandari kavu ya AMI.
Kamishna wa Ukaguzi na Sayansi ya Jinai kutoka kwenye mamlaka hiyo, Bertha Mamuya, alisema ukamataji wa makontena hayo ni mwendelezo wa tukio la ukamataji mwingine kama huo uliofanyika mwezi uliopita katika eneo la Mwenge, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akieleza zaidi kuhusu tukio hilo, alisema wakiwa katika ufuatiliaji, walipata taarifa ya kuwapo kwa mzigo huo wenye ujazo wa jumla ya lita 6,000.
“Tunayashikilia (makontena) mpaka uchunguzi utakapokamilika. Tunataka kujua kibali wamepata wapi na wameyaingizaje nchini wakati kibali chao kimeisha.

“Tulikuwa tunaandaa jalada lao la kesi ya awali ndipo tukapata taarifa hii… hivyo tunachunguza kubaini wamepata wapi kibali,” alisema kuelezea kemikali hizo ambazo hutumika kwenye viwanda na maabara kwa matumizi halali, lakini watu wasio waaminifu huweza kutumia kwa malengo mabaya ya kutengenezea dawa za kulevya.

No comments