Breaking News

Mchezaji huyu ashushwa Azam kwa dau la milioni 40

IMETHIBITIKA kuwa Klabu ya Azam imetumia milioni 40 kwa ajili ya kuipiku Yanga na kuinasa saini ya mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mbaraka Yusuph ambaye ametua ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Mromania, Aristica Cioaba hivi karibuni. 

Azam imemnasa Mbaraka aliyefunga mabao 11 katika msimu uliopita kwa ajili ya kuziba pengo la straika na nahodha wao, John Bocco aliyetimka na kumpa mkataba wa miaka miwili akitokea Kagera Sugar. 

Mmoja wa mabosi wa Azam, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, wametumia fedha hizo kwa ajili ya kumnasa Mbaraka ambaye alikuwa kwenye mawindo makali ya Yanga, kutokana na timu hiyo kumhitaji ndani ya kikosi chao. 

“Ishu ya kumnasa Mbaraka, ilibidi tufanye haraka kwani Yanga wenyewe walikuwa wakisubiri amalize mambo ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa inacheza na Lesotho, kisha ndiyo imfuate kwa ajili ya kumsainisha. 

“Lakini sisi kwa kulijua hilo, ndiyo maana tukaenda haraka na kumsainisha kwa milioni 40 na kumpa mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia timu yetu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ambao tumedhamiria kufanya vizuri na kurejesha heshima yetu.” 

Championi Jumatatu, lilimtafuta Mbaraka kuhusiana na ishu hiyo ambapo amesema kuwa alimalizana na Azam tangu Alhamisi iliyopita na alisaini kwa dau hilo la milioni 40. 

“Ukweli ni kuwa mimi nilisaini mkataba wa kutua Azam tangu Alhamisi iliyopita na kila kitu tulikimaliza siku hiyo, kwa sasa najiandaa kwa ajili ya kuhakikisha naifanikisha timu yangu ifanye vyema msimu ujao,” alisema.

No comments