SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amewashtua wabunge juu ya namna ya kumaliza utata kuhusu kodi ya magari chakavu
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amewashtua wabunge juu ya namna ya kumaliza utata kuhusu kodi ya magari chakavu kwa kuwataka wawasilishe marekebisho ya sheria ya umiliki na matumizi ya vyombo vya moto ili kuibana serikali iharakishe mchakato huo.
Hatua hiyo ya Spika Ndugai ilitokana na wabunge wengi kuitaka serikali ibadili sheria hiyo kwa kuwa imekuwa kero ya muda mrefu kwa wananchi wanaomiliki wa vyombo hivyo.
“Nyie wabunge mna nafasi ya kuleta mabadiliko ya sheria kama mbunge mmoja mmoja ama kama kamati ya bunge ili kuibana serikali iweze kuharakisha mchakato huu,” alisema Spika Ndugai.
Awali, miongoni mwa wabunge waliohoji suala hilo ni pamoja na Mbunge wa Busega(CCM), Dk.Raphael Chegeni ambaye katika swali lake la msingi alitaka kujua kama serikali haioni haja ya kurekebisha Road Licence au ifutwe ili ukusanyaji wa kodi hiyo uendane na matumizi halisi ya vyombo hivyo.
“Kuna baadhi ya watu wanasumbuliwa barabarani kwa kudaiwa madeni ya muda mrefu na gari haifanyi kazi ipo nyumbani na wadaiwa walipe kodi hiyo.Serikali ni kwanini isitoe tamko ili watu wasisumbuliwe barabarani kuhusu kodi hii,”alisema
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy, alisema kodi hiyo imekuwa kero kubwa kwa wananchi kwa kuwa wanatozwa huku baadhi ya magari yakiwa gereji kwa miaka mitatu.
"Mheshimiwa Spika mimi nina gari liko gereji mwaka wa tatu halipo barabarani, lakini bado natakiwa nilipe hiyo kodi na faini juu. Hii si sawa kwanini serikali isiweke kodi hii katika mafuta ili kuondoa kero," alisema Keissy.
Kwa upande wake, Mbunge wa Iringa mjini(Chadema),Peter Msigwa aliitaka serikali kuifuta kodi hiyo kwa kuwa imekuwa kero kwa wananchi.
“Ni tatizo kubwa sana gari halimilikiwi kila mwaka, tunalipa kwa ajili ya matumizi ya barabara na watu wamepata tabu katika hili kwanini serikali isitoe tamko ya kufuta ili ilipwe kutokana na matumizi ya barabara,”alisema Msigwa
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji, alisema serikali inatarajia kurekebisha sheria hiyo ili kupata njia bora zaidi ya kukusanya ada hiyo lakini kwa sasa itaendelea kulipwa kwa utaratibu uliopo.
Alisema serikali inatarajia kufanyia mapitio ya Sheria na Kanuni ya umiliki na matumizi ya vyombo vya moto na kwamba sheria haitoi fursa ya ada hiyo kufutwa kwa kuwa ipo kwa mujibu wa sheria.
"Nimesikia kilio cha wabunge na Watanzania wakizungumzia road licence… lakini kwa sasa siwezi kutamka kuifuta bila kuangalia upya sheria yetu," alisema Dk. Ashatu.
Alisema ada ya mwaka ya magari inatozwa kwa wamiliki wa vyombo vya moto kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 1973 (Road Traffic Act, 1973).
Alibainisha kwa mujibu wa sheria mmiliki wa chombo anatakiwa kulipa ada ya kila mwaka kulingana na ukubwa wa injini ya chombo kilichosajiliwa.
Dk. Kijaji alisema msingi wa tozo hiyo ni umiliki wa chombo na si matumizi ya chombo barabarani, hivyo mmiliki anatakiwa kulipa ada bila kujali kama chombo kimetumika katika mwaka husika au hakijatumika.
Alisema ada ya umiliki ya mwaka wa chombo cha moto inaweza kusitishwa kulipwa endapo mmiliki atatoa taarifa kwa Kamishna wa Kodi na kuthibitishwa hakitumiki kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo ajali au uchakavu.
Aidha, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema suala hilo serikali imelisikia suala hilo na litatamazwa kwa ujumla wake lakini haiwezekani kutoa tamko la kubadili sheria bila kuzingatia utaratibu wa kisheria wa kubadili sheria.
No comments