Breaking News

Kimenuka IPTL, mabosi wake kortini

Mfanyabiashara James Rugemalira (kushoto) na mmiliki wa Kampuni ya PAP, Habirnder Seth Singh wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana kabla ya kusomewa mashtaka ya makosa ya uhujumu uchumi. Habirnder Seth Singh (alivaa kitambaa kichwani) na mfanyabiashara James Rugemalira (wa pili kushoto) wakiwa chini ya ulinzi wa askari katika gari la polisi wakipelekwa gerezani jana. Picha zote na Ericky Boniphace

Wawili hao pia wameshtakiwa kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 wakiwa jijini Dar es Salaam, Afrika Kusini, Kenya na India.
Dalili za ukubwa wa kesi hiyo zilianza kuonekana jana wakati mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola alipoitisha mkutano na waandishi wa habari kuwaeleza uamuzi wa kuwafikisha wafanyabiashara hao mahakamani.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara maarufu nchini, James Rugemarila na Harbinder Seth Singh jana walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuhujumu uchumi katika moja ya kesi zinazotarajiwa kuvuta macho ya wengi.

Wawili hao pia wameshtakiwa kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 wakiwa jijini Dar es Salaam, Afrika Kusini, Kenya na India.

Dalili za ukubwa wa kesi hiyo zilianza kuonekana jana wakati mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola alipoitisha mkutano na waandishi wa habari kuwaeleza uamuzi wa kuwafikisha wafanyabiashara hao mahakamani.

Katika mkutano huo na waandishi, Mlowola alidokeza kuwa kwa muda huo wa mkutano, Rugemalira, aliyekuwa na hisa katika kampuni ya IPTL, na Harbinder, ambaye kwa sasa anaimiliki kampuni hiyo ya kufua umeme, walikuwa wameshafikishwa mahakamani.

“Ndugu wanahabari, leo tumewaita mchana huu ili kuwapa taarifa za mapambano yetu dhidi ya rushwa nchini. Na leo tunawapa taarifa kwamba tunawafikisha mahakamani watuhumiwa wawili. Bwana Harbinder Sing Seth na Bwana James Buchard Rugemarila,” alisema Mlowola katika mkutano huo wa aina yake na waandishi wa habari.

“Hawa tunawafikisha mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi na makosa mengine yanayofanana na hayo.”

Mlowola alisema amekuwa akiulizwa kwa muda mrefu kuhusu maendeleo ya kesi za uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow na sakata la IPTL.

Mlowola alisema kwa kuwa taasisi yake inahusika na kuzuia na kupambana na rushwa, imekuwa ikishughulikia masuala hayo.

“Kwa hiyo, katika muendelezo wa majukumu yetu, tulichunguza shauri hili kwa muda mrefu na sasa umefika wakati muafaka wa kuwafikisha watuhumiwa wakuu hawa wa mashauri haya ya kuhujumu uchumi wetu, mahakamani,” alisema Mlowola.

“Kwa hiyo, kwa wale walioenda mahakamani, tayari wameshapelekwa mahakamani. Na nitoe wito tu kwa wananchi kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kupambana na vitendo hivi vya uhujumu uchumi ili wananchi wapate maisha bora zaidi.”

Takriban kilomita nne kutoka eneo ambalo Mlowola alifanya mkutano mfupi na waandishi wa habari, wafanyabiashara hao walikuwa wakifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu wakishtakiwa kwa makosa sita ya uhujumu uchumi, likiwamo la kuisababisha Serikali hasara ya jumla ya takriban Sh358 bilioni.

Wakili wa Serikali, Paul Kadushi aliyataja mashtaka mengine yanayowakabili wawili hao kuwa ni kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu  na kuisababishia hasara Serikali.

Rugemarila, ambaye ni mkurugenzi wa VIP na aliyekuwa mmiliki mwenza wa IPTL, na Seth, ambaye ni mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP) inayomiliki IPTL, wanadaiwa kuwa walikula njama hizo kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam na katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Kadushi alidai katika shtaka la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao, wakiwa si watumishi wa umma waliunda mtandao wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Seth anadaiwa kuwa alighushi fomu namba 14 ya usajili wa kampuni na kuonyesha kuwa ni Mtanzania anayeishi Mtaa wa Mrikau, Kitalu Namba 887, Masaki jijini Dar es Salaam, uongo anaotuhumiwa kuufanya Oktoba 10, 2011.

Seth anadaiwa kutoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14a ya usajili wa kampuni kwa ofisa msajili wa kampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Washtakiwa wote wanadaiwa kujipatia kwa ulaghai kutoka Benki Kuu (BoT) dola 22,198,544.60 za Kimarekani na Sh309,461,158.27 za Kitanzania kati ya Novemba 28, 29 mwaka 2011 na Januari 23, 2014 wakiwa makao makuu ya benki ya Stanbic Kinondoni na benki ya Mkombozi, tawi la St Joseph.

Kiasi hicho cha fedha kimewafanya wawili hao washtakiwe kwa kosa jingine la kuisababishia Serikali hasara kwa tukio lililotokea Novemba 29, 2013 katika tawi la Kati la benki ya Stanbic.

Seth na Rugemarila watalazimika kulala mahabusu hadi Julai 3 baada ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kukubaliana na hoja za upande wa mashtaka za kutaka washtakiwa hao wasipewe dhamana kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka katika kesi za uhujumu uchumi.

Awali, wakili wa utetezi, Respicius Didas aliomba mahakama iwape wateja wao dhamana akisema mashtaka yao yanadhaminika, lakini Wakili Kadushi alieleza chombo chenye mamlaka ni Mahakama Kuu na ndiyo maana washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote baada ya kusomewa mashtaka.

Alisema mazingira pekee ambayo yangeifanya mahakama iweze kusikiliza ni pale ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anapotoa cheti maalumu cha kuipa mamlaka hayo Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi hiyo.

No comments