Abiria 75 wanusurika kifo basi likiteketea kwa moto
Basi la kampuni ya Batco hufanya safari kati ya Sirari na Mwanza.
Butiama. Basi la kampuni ya Batco lililokuwa likitokea Sirari kuelekea Mwanza muda mfupi baada ya kuvuka Mto Mara lilianza kufuka Moshi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Jaffari Mohamed akizungumzia tukio hilo amesema wanafuatilia kubaini chanzo cha ajili hiyo iliyosababisha mali za abiria kuteketea kwa moto, huku abiria 75 waliokuwamo wakinusurika kifo.
Basi hilo lilianza kuteketea moto leo (Jumamosi) saa saba mchana eneo la Kirumi, Kata ya Bukabwa wilayani Butiama.
Chanzo cha kuteketea basi hilo hakijajulikana, huku zaidi ya abiria 75 waliokuwa ndani wakinusurika.
Mmoja wa abiria hao, mwalimu Malakwa Asenga amesema basi lilianza kuonyesha kuwa na hitilafu walipokuwa wakitoka mjini Tarime.
Amesema dereva aliendelea na safari na walipofika eneo la Mto Mara alisimama kwa muda akiwa ameegemea usukani na baadaye aliondoka.
Asenga amesema hawakufika mbali dereva alisimama tena, ndipo walipoona moshi ukitoka kwenye injini.
Abiria huyo anasema alimwambia mwenzake washuke kwa kuwa gari linaungua.
“Nikisema hayo tayari abiria wengine walikuwa wameanza kushuka kwa haraka wakiwa na mizigo yao ili kuokoa maisha lakini moto ulikuwa umeanza kuongezeka hivyo ni mizigo michache tu ndiyo iliyookolewa, yangu imeteketea,” amesema Asenga.
No comments