SHIRIKA LA AGPAHI LAFUNGA KAMBI YA WIKI MOJA YA WATOTO KUTOKA MARA,SIMIYU NA TANGA JIJINI MWANZA
Meneja wa shirika la AGPAHI kanda ya Ziwa Victoria,Dkt. Nkingwa Mabelele akitoa hotuba katika sherehe za kufunga kambi ya watoto jijini Mwanza.
****
SHIRIKA lisilo la kiserikali la AGPAHI limewasihi watoto kuzingatia masomo, kanuni za afya kama zinavyoelekezwa na wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja kuwahamasisha watoto wengine kujiunga katika vikundi vya watoto.
Rai hiyo imetolewa leo na Meneja wa kanda wa Shirika hilo Dkt. Nkingwa Mabelele wakati wa kufunga kambi ya watoto iliyoandaliwa na shirika hilo iliyojumuisha watoto kutoka mkoa wa Mara, Simiyu na Tanga wenye umri kati ya miaka 9 mpaka 17.
Dkt. Mabelele alisema elimu ni msingi kwa kila mtoto hivyo watoto wanatakiwa kusoma kwa bidii na kuzingatia yale wanayofundishwa ikiwa ni pamoja na kufuatilia kanuni za Afya wawapo shuleni na nyumbani.
Dkt. Mabelele alibainisha kuwa ,Shirika la AGPAHI limeendelea kutoa huduma za kisaikolojia kwa kupitia vikundi vya watoto na kwamba vikundi hivyo vipo katika vituo vya kutolea huduma za Afya za CTC.
Awali katika risala yao, watoto hao walilishukuru Shirika la AGPAHI kwa kuwaandalia kambi hiyo kwani imewasaidia kujifunza mambo mengi ya afya, makuzi, lishe, usafi binafsi pamoja na kufahamiana.
Aidha wameiomba serikali iliunge mkono shirika la AGPAHI ili huduma za kisaikolojia kwa watoto kwa kupitia vikundi ziendelezwe na kuwafikia watoto wengi nchini.
Kwa upande wake, msaikolojia aliyekuwa na watoto kambini kwa muda wa wiki moja amewataka wazazi kuwasikiliza watoto na siyo kuwapiga na kuwatukana kwani kwa kufanya hivyo kutasababisha watoto wajisikie wanyonge na wasiothaminiwa.
Shirika la AGPAHI lilianzishwa mwaka 2011, hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu shirika limefanikiwa kuwafikia jumla ya watu 189,806 kupata huduma za VVU/Ukimwi ikiwemo kupata dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV) na kati ya hao watoto wakiwa 8,615 sawa na asilimia 5%.
No comments