Aliyetobolewa Macho na Scorpion… Asimulia Yakukutoa Machozi!
DAR ES SALAAM: Majanga upya! Unaweza sema hivyo kwa maana nyingine baada ya yule kijana aliyetobolewa macho, Said Mrisho kufunguka mambo mazito ya kukutoa machozi ya kinachoendelea ikiwa miezi michache imepita tangu apatwe na ulemavu huo, Ijumaa linakuhabarisha!
Mapema wiki hii saa chache baada ya kesi yake dhidi ya Scorpion kuahirishwa, waandishi wetu walikutana na Said nyumbani kwao, MabiboHosteli na kuzungumza naye mambo mengi huku akiweka wazi kilio chake kwa mambo mengi ya kuhuzunisha yanayoendelea maishani mwake kwa sasa.
Said anasema tangu apate ulemavu huo, bado anayo maumivu ya macho, ambapo mishipa humsimama na kusababisha maumivu makali hali inayomlazimu kumeza dawa kila siku kabla ya kulala. “Kuna mishipa inayounganisha macho na ubongo, bado inafanya kazi, sasa unakuta inalazimisha kupeleka eneo la macho ile nguvu ya kuona vitu, lakini macho hayana uwezo huo na hapo ndipo maumivu makali huanza upya, kila siku nalazimika kunywa dawa kabla sijalala, kifupi bado naumwa jamani, lakini bado ninayo imani na matumaini ya kupona.
“Wanangu wananiumiza mno, kila siku hawaachi kuuliza nitaona lini, kuna kipindi nilisafiri kwenda Moshi, nilivyorudi watoto wangu walijua nilienda kuwekewa macho mengine, wakajua nitakuwa naona, maswali yakawa mengi, niliumia sana,” anasema Said kwa uso wa masikitiko na majonzi.
Salum Njwete ‘Scorpion’
Said anaendelea kusimulia kuwa, hata saluni kwake alipokuwa akifanya kazi mambo yameharibika maana hata mauzo yanashuka. “Wakati nikiwepo nilikuwa nacheka na kila mtu, hivyo mapato yalikuwa mengi lakini sasa hivi hakuna kabisa wateja, tumeshabadilisha wafanyakazi wengi mno lakini hawamuoni mtu waliyemzoea.”Akizungumzia misaada aliyopewa ikiwemo pikipiki na Bajaj Saidi anasema;
“Nilipewa msaada wa pikipiki tano, ambazo nne zinafanya kazi na moja bado iko hapa haijapata dereva, Bajaj ni mbili na zote zinafanya kazi, kwa upande wa pikipiki tulielewana wawe wananiletea shilingi 10,000/= kila siku, wakaomba wawe wanaleta kwa wiki, lakini wakati mwingine inafika wiki hawaleti au wanakuja na pesa kidogo mno wakidai hali ni ngumu, wale wa Bajaj nao usumbufu ni uleule, tabu kwelikweli, maana wanajua niko katika hali ambayo siwezi kuwasimamia kwa ukamilifu, nabaki naumia tu!”
Said akiwa na familia yake.
Said anaendelea kusema kwa masikitiko kuwa, kitu kikubwa kinachoendelea kumuumiza
hadi sasa ni suala la makazi kwani miongoni mwa mambo aliyoahidiwa ni nyumba, huku msimamizi mkuu akiwa mkuu wa mkoa ambaye hadi sasa anaonekena kutokuwa na ushirikiano naye.
“Hata ile pesa shilingi milioni 10 niliyopewa inazidi kuyeyuka kwa kulipa kodi ya pango na matumizi ya kifamilia, kuna kipindi nilimueleza mkuu wa mkoa, akaniambia nilipie mwezi mmoja tu maana nyumba iko tayari na muda wowote ningekabidhiwa, hapo ilikuwa mwaka jana mwezi wa 11, nikalipa mwezi mmoja lakini bado hakuna kilichoendelea.
“Baadaye ikanibidi nilipie miezi sita, nayo ikaisha na sasa nimelipa miezi mitatu na kodi inaisha mwezi wa saba, sina mahali pa kushika na nyumba sijakabidhiwa, wale watu walioambiwa na mkuu wa mkoa kunipatia nyumba, wanasema iko tayari lakini wanasubiri amri kutoka kwa mkuu, siku hizi hata mawasialiano naye si kama zamani, hapokei simu zangu na hata nikimtumia meseji ya sauti kati ya nne anajibu moja, sijui itakuwaje jamani!” Alisema Said kwa sauti yenye huzuni.
No comments