Breaking News

KOCHA YANGA AITAKA NAFASI YA PLUJIM SINGIDA UNITED


Imebainika kuwa aliyewahi kuwa Kocha wa Yanga, Du­san Kondic, raia wa Serbia ni miongoni mwa makocha ambao wanapigiwa chapuo kwa ajili ya kwenda kuchukua mikoba ya Mholanzi, Hans van Der Pluijm ambaye ataondoka kwenye kikosi cha Singida mwishoni mwa msimu huu.

Singida United watalazimika kutafuta kocha mpya ambaye atarithi viatu vya Hans Pluijm ambaye tayari ameshafunga mahesabu ya kuifundisha timu hiyo ambayo alisaini nayo mkataba wa miaka miwili. Mdachi huyo inatajwa kuwa anaenda kujiunga na timu ya Azam FC.

Kwa mujibu wa Gazeti la Championi limeeleza kuwa jina la kocha huyo Mserbia ambaye kwa sasa amejikita nchini Afrika Kusini ambapo mara ya mwisho alikuwa akiifundisha Royal Eagles ya Ligi Kuu ya Ufaransa limo kwenye orodha ya majina ya makocha wengi ambao tayari wamewasilisha wasifu wao (CV) kwa ajili ya kuinoa timu hiyo.

“Tayari kuna makocha wengi ambao wamejitokeza kwa ajili ya kutaka ku­chukua mikoba ya kocha Pluijm ambaye ameshatangaza nafasi ya kuondoka itakapofika mwisho wa msimu, moja ya majina hayo ni Dusan Kondic ambaye alikuwa Yanga.

“Siyo yeye tu kuna orodha ndefu ya makocha pia akiwemo Mrundi Ettiene Ndayiragije ambaye pia naye anatajwa kwa kiasi kikubwa kuja kuwa kocha hapa kwa msimu ujao ikiwa ni baada ya kuondoka kwa Pluijm,” kilisema chanzo hicho.

Championi lilimuuliza Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga ambaye alisema: “Tuna majina na CV nyingi za makocha ambao wameomba kuja kuwa na sisi, huyo ni miongoni mwao, lakini kwetu hatutaangalia ni kocha mzawa au mgeni bali tutaanga­lia uwezo wa kocha ambaye atatufanya tufanye vizuri katika michuano ya kimataifa.”

No comments