Breaking News

Wapinzani wa Singida United watuma salamu

Klabu cha JKT Tanzania FC imeingia kambini leo kujiandaa na mchezo wake wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Singida United kati ya Aprili 16 na 18, mwaka huu.

Timu hiyo iliyopanda tena Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara msimu ujao, ilifanikiwa kuingia katika hatua hiyo baada ya kuiondoa Tanzania Prisons katika robo fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya Jumamosi iliyopita.

Kocha Mkuu wa JKT, Bakari Shime amesema anatambua wapinzani wao hao sio wa kubeza hivyo anawatengeneza vijana wake kwa ajili ya kuhakikisha wanaendeleza kiwango kile kile katika hatua hiyo ya nusu fainali.

''Tunatarajia kwenda nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, kwa ajili ya kuweka kambi na kufanya maandalizi yetu ili kuhakikisha tunafanya vyema dhidi ya Singida United, hakuna timu ambayo tutaibeza, ukizingatia wenzetu wako katika ligi”, amesema.

Nusu fainali nyingine ya Kombe la shirikisho itazikutanisha Mtibwa Sugar ya Morogoro na Stand United ya Shinyanga kati ya Aprili 16 na 18 pia mwaka huu.

No comments