Askofu Kakobe: Nipo Tayari Kufa Hakuna Atakayenizuia Kusema Ukweli
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe amesema licha ya kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji kuhusu uraia wake, yupo tayari kufa kwa kusema ukweli na hakuna mtu atakayemzuia kufanya hivyo.
Akizungumza na Amani mara baada ya kuhojiwa na maofisa wa Uhamiaji Jumatatu iliyopita, Askofu Kakobe alisema yeye ni mhubiri wa kweli wa neno la Mungu na hakuna kitakachomtenganisha na wito huo.
Akizungumzia uraia wake ambao ulimfanya ahojiwe, Askofu Kakobe alisema yeye anatoka katika Kijiji cha Mbizi katika wilaya mpya ya Kakonko na familia yao ni maarufu sana na kwa makusudi kabisa baba yake alipofariki dunia mwaka 2009 na mama yake alipofariki dunia mwaka 2013 alitoa maelekezo kwamba makaburi hayo yawekwe mbele ya nyumba yao kwa sababu yeye ni mtu wa kusema ukweli.
Kiongozi huyo wa kiroho alisema anashangaa kuona sasa anahojiwa na akahoji kwa nini iwe sasa? Akasema zoezi la kuangalia uraia lingekuwa la watu wote kusingekuwa na maswali.
Hata hivyo, alisema kama hakuna uovu na hakuna kilichofichika itabidi huyo anayesema yeye siyo raia wa hapa aseme ni wa nchi gani na atoe vithibitisho.
“Katika nchi nyingine wenzetu wanasema I’m proud of my country, I’m proud of my nation (nina fahari na nchi yangu, nina fahari na taifa langu), mtu anaona fahari kuitwa raia wa nchi hiyo na ukizungumza kuwa huyu siyo raia, sidhani kama hivyo ni vitu vya afya katika jamii,” alisema Askofu Kakobe.
Alisema anashangaa kwa nini wanaohojiwa uraia wengi ni kutoka Mkoa wa Kigoma akahoji je, ni makosa kuzaliwa katika mikoa ya mpakani?
Alibainisha kuwa yeye ana hati ya kusafiria moja na ameitoa mara nne (baada ya kujaa moja baada ya nyingine) na kwamba amewaachia maofisa wa uhamiaji ili waangalie ‘afidaviti’ zake, (hati za viapo) ambazo zilitakiwa katika maelezo yake.
Alisema aliulizwa kuhusu cheti cha kuzaliwa lakini akawaambia kwamba yeye alizaliwa mwaka 1955 na wakati huo kulikuwa hakuna vyeti hivyo.
No comments