Breaking News

Askofu anusurika Kukatwa mapanga kanisani

Askofu  Wilberforce Luwalira wa Kanisa la Roma la Mtakatifu Paulo, Namirembe nchini Uganda  alinusurika kifo baada ya Herbert Kadu (35), kuibuka ghafla kanisani akiwa ameshika panga na kumkimbilia nalo madhabahuni wakati ibada ya Pasaka ikiendelea.

 Tukio hilo la aina yake lilitokea juzi nchini Uganda wakati Askofu Luwalira akiendesha ibada ya Pasaka kanisani hapo.

Ujumbe wa video fupi uliosambaa jana kwenye mitandao ya kijamii unaonyesha ibada hiyo ikiendelea,  ghafla Kadu akiwa amebeba panga alianza kumkimbilia eneo la madhahabuni alikokuwa askofu huyo.

Kabla ya kumfikia askofu huyo, Kadu alijaribu kuruka kizingiti kilichotenganisha eneo la madhabahu na waumini na katika jitihada hizo alianguka na kukamatwa na wasimamizi na waumini ndani ya kanisa hilo.

Kijana huyo alijaribu kuruka kizingiti ili kwenda kwa askofu ambaye wakati huo alikuwa amesimama na msaidizi wake wakiendelea na ibada, na baada ya kuruka alidondoka upande wa madhahabu.

Wasaizidi wa askofu huyo walimdhibiti kijana huyo na kumbeba kumwondoa ndani ya kanisa hilo ili asitekeleze kusudio lake.

Taarifa zilizopatikana kanisani hapo zilisema kijana huyo aliwasili kanisani hapo akiendesha gari aina ya 'kipanya' Super Custom na kuegesha lango kuu la kuingilia kanisani hapo.

“Alipoingia alimpiga mlinzi wa getini na kuingia kwa nguvu kanisani na alikaa kanisani muda mrefu hadi ibada ilipokaribia kuisha ndipo alipojaribu kwenda madhabahuni,” shuhuda alisema katika video hiyo.

Taarifa ilisema baadaye askari walimkamata na kumpeleka kituo cha polisi Namirembe kwa mahojiano.


No comments