Breaking News

LISSU ASIMAMA BILA MAGONGO, KUFANYIWA UPASUAJI MWINGINE JUMATANO

Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, anatarajia kufanyiwa upasuaji mwingine katikati ya wiki ijayo,

Kwenye taarifa yake kwa Umma aliyoitoa jana, Lissu alieleza kuwa mguu wake wa kulia ambao uliathirika sana sasa unaendelea kupata nguvu na anaweza kusimama kwa miguu yote bila msaada wa magongo,

Lissu aliendelea kueleza kuwa Timu ya Madaktari Bingwa wa Mifupa wanaomtibu, wamemtaarifu kwamba kasi ya kuunga kwa mfupa wa juu ya goti ni ndogo sana,

"Madaktari wangu wamesema kwamba wasipoingilia kati na kurekebisha mfupa huo, kwanza itachukua muda mrefu sana kuunga, na pili, hata ukiunga baada ya huo muda mrefu, hautaunga kwa namna itakayoondoa hatari ya kuvunjika siku za mbeleni,” alieleza Lissu

Mbunge huyo anasema kuwa kwa sababu hizo hapo juu, Madaktari wake wamependekeza kufanyika Upasuaji mwingine kwenye mfupa wa juu ya goti la kulia,

“Wameniambia kuwa siku ya Jumatano ijayo ya Machi 14, nitarudi Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg, kwa ajili ya kufanyiwa Upasuaji huo,” alieleza Lissu

Mbunge huyo wa Singida Mashariki, anasema yupo kwenye mikono salama ya kitabibu chini ya Madaktari Bingwa wa Mifupa wakiongozwa na Profesa Dkt. Stefa Nijs na Profesa. Dkt. Willem-Jan Mertsemakers, 

Tundu Lissu anapata matibabu nchini Ubelgiji alikohamishwa kutoka Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa na Risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 nyumbani kwake mjini Dodoma

No comments