Breaking News

Hali ya taharuki yatanda kwa familia nne Dar

Katika hali isiyokuwa ya kawaida leo Mtaa wa Kibasila, Kata ya Upanga Mashariki , Wilayani Ilala,  jijini Dar es Salaam, kundi la mabaunsa wamevamia nyumba wanayoishi wanawake na kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji.

Mabaunsa hao inadawa walitumwa na kanisa moja (jina linahifadhiwa kwa sababu maalumu) ili kuziondoa kinguvu familia nne zinazoishi katika nyumba hizo  zilizokuwa mali ya Shirika la Maendeleo  Tanzania (NDC).

Inaelezwa, mabaunsa hao walivamia nyumba hiyo  majira ya saa 1:30 asubuhi  na kukuta baadhi ya wanawake wakiwa wamelala ambapo walivunja milango ya vyumba na kuwadhibiti huku wakiwapekua maungoni wakijifanya kutafuta simu.
Inaelezwa,  walipekua katika droo na kupora vito, fedha na mali  za thamani huku wakiwatishia kutokupiga simu mahari popote.

Mabaunsa hao walisomba samani za ndani  na kuzitupa umbali wa mita 15  nje ya nyumba hiyo, kuvunja baadhi ya vitu na kumwaga chakula.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibasila, Upanga Mashariki,  Rukia Liyami,  ambaye pia ni anaishi katika nyumba hiyo ameliita tukio hilo ni la kinyama.

Alisema, mabaunsa hao hawakujitambulisha walikotokea na wengi walikuwa wananukia harufu ya pombe.

“Hii nyumba tunaishi wanawake tupu na hawa waliokuja ni wanaume. Wameingia katika vyumba na kutudhalilisha. Huu ni unyama. Tunaomba  sheria ichukue mkondo wake,”alisema Rukia.

Alisema,   nyumba  hizo zilikuwa ni mali ya NDC na , ziliamriwa ziuzwe kwa wakazi waliomo ndani ya  nyumba hizo  lakini baadaye ziliuzwa kwa kanisa kinyume cha maelekezo hivyo wakazi wa nyumba hiyo kwenda mahakamani mwaka 2008 kupinga nyumba hizo kuuzwa kwa watu ambao si wakazi na kesi bado inaendelea Mahakama ya Rufaa.

“Ni swa  wamekuja kututoa ila serikali ipo,  wangetoa barua kwa serikali, Ofisa Mtendaji na Polisi wapo  mbona hawakujulishwa?” alihoji Rukia.

Aizi Mkindi alisema; “Walipoingia tuliwauliza wanahati zozote za  kutoka mamlaka husika? Wakadai wametumwa na kanisa na nyumba ni mali yao.
Tuliwauliza  vitambulisho vyao, walikataa kuonyesha na kuanza kututishia maisha,”alisema Mkindi.

Salma Abdalah alisema; “Tulijua tumevamiwa na majambazi. Muonekano wao ulikuwa kama vibaka wazoefu.

Nilijaribu kukimbia walinikamata na kunidhibiti kisha wakaanza kunipora simu yangu ya mkononi.

Nilimpasia mdogo wangu  mtoto  ili akimbie naye.Niliporejea ndani nilikuta wameingia chumbani kwangu wakipekua na kuiba,”alisema.

Aliongeza; “Katika pochi langu kulikuwa na sh.500,000 na seti mbili za dhahabu ambazo nilipewa kama zawadi yangu ya harusi,”

Mjumbe  wa Serikali ya Mtaa huo, Sadiq Mohammed Ally,  aliliita tukio hilo ni la fedheha hivyo kuiomba serikali kuingilia kati.

“  “Familia nne hazina mahari pa kuishi vyombo vimeharibiwa na kutupwa nje,
mimi kama mjumbe wa serikali ya mtaa huu sina taarifa yoyote na hakuna hati yoyote iliyotolewa kama wametoka mahakamani au mamlaka yoyote. Hatua kali lazima zichukuliwe,”alisema Ally.

Kamanda wa Polisi Mkoa Maalumu wa Kipolisi, Salumu Hamduni, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Tukio tunalo na  bado suala lipo katika  uchunguzi,”alisema Kamanda Hamduni.

Aliongea, sisi polisi tunasimamia amri halali za mahakama, kama kungekuwa na agizo lolote tulilipaswa kuletewa taarifa. Ofisi  yangu hainataarifa  ya amri ya utoaji mali katika nyumba hizo,”

Alisema kama hakukuwa na taarifa basi tukio hilo limefanyika  kinyume cha sheria au hawakuona  umuhimu wa polisi kushirikishwa.

Hamduni alisema tayari wanamshikilia mtuhumiwa mmoja aliyeshiriki na wanaendelea kumhoji huku msako kwa wahusika wengine ukiendelea.

No comments