CHADEMA WAMJIBU MSAJILI WA VYAMA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimejibu barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi inayowataka ndani ya siku tano kuwasilisha maelezo ya tuhuma za uvunjifu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na ya maadili ya vyama vya siasa kwa kufanya maandamano Februari 16, 2018.
Katika majibu yake, Chadema wamejibu hoja mbalimbali za msajili na kuhoji hatua alizochukua mpaka sasa kufuatia mfululizo wa matukio ya mauaji ya viongozi wa chama hicho.
Akizungumza leo Februari 23, 2018 na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho-Bara, John Mnyika amesema msajili kwenye barua yake anakituhumu Chadema kwa kukiuka kifungu cha 9(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa.
Mnyika amefafanua kwamba kifungu hicho hakihusu vyama vyenye usajili wa kudumu bali vyama vya siasa vyenye usajili wa muda mfupi ambavyo vinaahidi kwamba vikipata usajili wa kudumu vitadumisha amani katika shughuli zao.
Mnyika amekosoa pia barua ya msajili ambaye anahoji ushiriki wa Chadema kwenye uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Ubungo wakati uchaguzi huo ulifanyika katika jimbo la Kinondoni, kuongeza kuwa hiyo inaonyesha kwamba msajili amekosa umakini katika majukumu yake.
"Tunaelewa kwamba msajili anasukumwa na Serikali. Dhamira yao ni kukifuta Chadema. Nawaambia tu jambo hilo hawaliwezi," amesema.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Kibamba amesema msajili amebainisha kwenye barua yake kwamba wamekiuka kanuni ya 6(1)(b) ya maadili ya vyama vya siasa ambayo inampa mamlaka ya kupokea malalamiko na kuzisikiliza pande mbili.
Akijibu jambo hilo Mnyika amesema msajili hajabainisha mlalamikaji ni nani katika malalamiko aliyoyapokea.
Chama hicho pia kimelaani mauaji ya diwani wake Kata ya Namala, Godfrey Luena na kutaka Polisi kufanya uchunguzi wa haraka na kumchukulia hatua za kisheria kila anayehusika.
"Katika Taifa letu kwa sasa, kuna vikundi vya watekaji, vikundi vya wauaji na vikundi vya watesaji. Ni wakati wa kujilinda kwa sababu kuna mashambulizi mengi sana," amesema Mnyika.
No comments