Breaking News

SAFARI YA RAIS MAGUFULI KUHAMIA DODOMA YAIVA

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais John Magufuli atahamia Dodoma wakati wowote mwakani na si 2020 kama ilivyotangazwa awali.

Pia, amesema Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan atahamia Dodoma mwishoni mwa mwaka huu na kwamba maandalizi kwa ajili hiyo yapo tayari.

Waziri Mkuu alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) mjini hapa. Alisema hadi sasa watumishi 2,346 kutoka wizara zote wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi wameshahamia Dodoma.

Waziri Mkuu alisema kumekuwa na visingizio mbalimbali kwa watumishi ikiwamo shule kwa watoto kama kikwazo cha wao kuhamia Dodoma jambo alisema halina mashiko kwa sasa.

“Dodoma inazo shule nzuri zinazofaa kufundisha watoto wa viongozi ikiwamo vyuo vikuu vikubwa ndani ya Afrika Mashariki. Kusiwepo kisingizio tena,” alisema Majaliwa.

Juzi, Majaliwa alikagua matengenezo ya makazi ya muda yanayotarajiwa kutumiwa na Makamu wa Rais eneo la Kilimani ambayo awali yalikuwa makazi ya mkuu wa mkoa.

Rais John Magufuli alitangaza Serikali kuhamia Dodoma katika sherehe za Sikukuu ya Mashujaa zilizofanyika kitaifa kwa mara ya kwanza mjini humo mwaka 2016.

Baada ya uamuzi huo, Waziri Mkuu alitoa ratiba ya namna Serikali itakavyohamia katika kipindi cha miaka mitano huku mwenyewe akiwa wa kwanza kuhamia Septemba Mosi, mwaka jana.

Alisema ratiba ya Serikali kuhamia Dodoma ilianza Septemba 2016 na kwamba ingekamilika mwaka 2020 wakati nchi itakapofanya Uchaguzi Mkuu.

Mbali ya Majaliwa, awamu ya kwanza ya kuhamia Dodoma iliwahusisha pia mawaziri wote, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na baadhi ya idara na ilianza Septemba 2016 hadi Februari.

Awamu ya pili ilikuwa kati ya Machi hadi Agosti ikiwahusisha watendaji wa wizara mbalimbali. Awamu ya tatu ilianza Septemba na itakamilika Februari mwakani na ya nne itaanza Machi na kukamilika Agosti.

Awamu ya tano imepangwa kuanza Septemba mwakani hadi Februari 2020 ambayo itakuwa kuhamisha watumishi wa wizara waliobakia jijini Dar es Salaam na awamu ya sita awali ilipangwa kuanza kati ya Machi 2020 hadi Juni ambako Ofisi ya Rais ikiongozwa na Rais, Makamu wa Rais wangehamia Dodoma kabla ya mabadiliko hayo yaliyotangazwa jana na Waziri Mkuu.

No comments