Breaking News

POLISI WAKERWA WIZI WA MAFUTA YA TRENI TAZARA

KAMANDA wa Polisi Kikosi cha Tazara, Patrick Byatao amesema wafanyakazi wasio waaminifu wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) wanalisababishia hasara shirika hilo kutokana wizi wa mafuta katika treni.

Akizungumza katika hafla ya kuwapa zawadi wafanyakazi bora 10 wa mwaka 2017, Dar es Salaam jana, Kamanda Byatao aliyataja maeneo korofi ambayo wizi huo hufanyika kuwa ni pamoja na stesheni ya Mlimba (Kilombero), Makambako (Njombe), Kongaga (Mbarali), Mpemba (Songwe) na Tunduma.

Alisema watumishi hao hususani madereva wamekuwa wakishirikiana na wananchi kuiba mafuta na ndiyo maana shirika hilo haliendelei. Kamanda Byatao alisema kuwa Oktoba 7, mwaka huu, walifanikiwa kumkamata dereva wa treni, Kagwa Ruoga na Mathew Mkula ambao walikuwa wakiendesha treni lililobeba shaba kutoka Zambia kwenda Dar es Salaam na kwamba huku treni hilo likiwa linatembea waliingiza watu watano na kuanza kuchukua mafuta ya dizeli.

Aliwataka wananchi kutoshiriki katika matukio hayo ya uhalifu na kwamba watumishi hao watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuhujumu uchumi. 

Aidha, aliwataka askari hao kufanya kazi kwa uadilifu na kuwa wadadisi ili kugundua matukio mbalimbali ambayo yanaweza kuhatarisha maisha.

Mmoja wa askari waliopata zawadi, Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Tazara, Insepkta Halid Kingazi alisema kuwa wataendelea kupambana na uhalifu ili kuhakikisha wizi unaofanywa unaisha na shirika kubaki salama.

Kingazi alisema kuwa waendesha mashitaka wanapaswa kuwapa ushirikiano kwa kuhakikisha kesi wanazozipeleka mahakamani zinakwisha kwa wakati. 

Kikosi hicho kimetoa zawadi kwa askari wake walipo makao makuu Tazara, Kituo cha Mlimba Kilombero na Iyunga Mbeya ambapo treni hiyo inapita.

No comments