Breaking News

NDOTO ZA MBWANA SAMATTA: ZINAANZA KUTIMIA



Mchezaji huyo wa kimataifa wa Tanzania ameanza kufanikiwa Genk tangu atue klabuni hapo akitokea TP Mazembe
Mbwana Samatta amesema anahisi kwamba ndoto zake sasa zinaanza kuwa halisi baada ya kuorodheshwa katika wachezaji 30 wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka Afrika.
Mshambuliaji huyo wa Genk aliiambiaGoal kwamba anafurahi sana kuona jina lake miongoni mwa wanaowania tuzo hiyo na jambo hilo limeongeza imani yake kuwa anachofanya si kazi bure na anapiga hatua zaidi kuelekea kutimiza ndoto zake.
"Ninafurahi sana kuona jina langu kati ya waliopendekezwa, sasa nimeamini kwamba jitihada zangu zimezaa matunda, na ndoto zangu zitakuwa kweli hivi karibuni na nadhani wachezaji wenzangu wa Tanzania wanaweza kujifunza kitu kutoka katika hili," alisema Samatta. 
Licha ya hayo, Samatta alipata majeraha ya mguu Jumamosi wakati klabu yake, KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Lokeren katika mchezo wa First Division A ya Ubelgiji uliopigwa katika dimba Luminus Arena.
Nyota huyo sasa yu shakani kucheza mechi ya kimataifa dhidi ya Benin wiki ijayo.
Nahodha huyo wa Taifa Stars alisema kuwa alipanga kujiunga na timu ya Tanzania Benin, lakini anasubiri taarifa ya daktari wa klabu yake kabla ya kufanya chochote.
"Sasa nasubiri taarifa ya daktari wa klabu yangu baada ya kupata majeraha jana, kisha nitajua kama nitaweza kuungana na Taifa Stars au la!".
Mbwana Samatta amecheza mechi yake ya 70 akiwa Genk, lakini alicheza dakika 40 kwani nafasi yake ilichukuliwa Nikolaos baada ya kupata majeraha.

No comments