Wapinzani wazungumzia mikutano ya hadhara wakiwa Ikulu
Wote wawili walitaja “mikutano ya hadhara” wakati walipokuwa wakikamilisha ushauri wao mfupi wakati wa hafla ya kutunuku wajumbe wa kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza mchanga wa madini unaosafirishwa nje, biashara, sheria na mikataba ya madini.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba jana waliibua suala la mikutano ya hadhara wakati walipopewa nafasi ya kuzungumza katika hafla ya Rais iliyofanyika Ikulu.
Wote wawili walitaja “mikutano ya hadhara” wakati walipokuwa wakikamilisha ushauri wao mfupi wakati wa hafla ya kutunuku wajumbe wa kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza mchanga wa madini unaosafirishwa nje, biashara, sheria na mikataba ya madini.
Wakati Profesa Lipumba alisema ametumia nafasi hiyo kutoa yake kwa kuwa mikutano ya hadhara imezuiwa, Cheyo alisema hawezi kuzungumza mengi kuepuka kuonekana amegeuza fursa hiyo kuwa mkutano wa hadhara.
Cheyo alijirudi baada ya kutumia muda mrefu zaidi ya Profesa Lipumba, akijikita katika kueleza kilio cha muda mrefu cha kutaka Serikali ifungue macho na kuchukua hatua ili rasilimali za nchi ziweze kusaidia Watanzania.
“Kuna siku moja nilikuwa , nikawaambia wazungu tumechoka kuitwa masikini. Huwezi ukawa masikini wakati una gesi ya ujazo wa 57 trilioni, na madini na kila kitu, halafu unaitwa masikini. Tumechoka,” alisema Cheyo.
“Wewe (Rais) umetusaidia kuondoka katika kuchoka huku. Asante sana Mheshimiwa Rais.”
Cheyo alitumia nafasi hiyo kumuomba Rais awaamini Watanzania kwa kuwa nchi ina watu wengi wenye akili.
“Tanzania ina watu wenye bongo, na ndio maana inaitwa Bongoland,” alisema huku akishangiliwa.
Hata hivyo aligeukia suala la siasa akitaka vyama visigeuze iviepuke vurugu.
“Nawaomba rafiki zangu ambao tuko katika vyama vya ushindani, hesbu tusigeuze mfumo huu wa vyama vingi kuwa kiwanda cha chuki,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Bariadi Mashariki.
“Mwalimu (Julius Nyerere) aliyefanya kila nguvu kuwaambia wana-CCM-- pamoja na asilimia 20 kusema tuwe na vyama vingi- tuwe na vyama vingi.
“Nia yake haikuwa kutengeneza kiwanda cha kutukanana, kiwanda cha chuki, kiwanda cha kukosa uzalendo. Vyama vya siasa tuwe kiungo cha Watanzania wote kushirikiana na uongozi ambao umechaguliwa kidemokrasia, kuongoza nchi yetu kwa sababu nchi hii itaendeshwa na sisi wote. Na wote tuna nafasi.”
Naye Profesa Lipumba alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais kwa kulipa kipa umbele suala la madini ambalo wamekuwa wakilipigia kelele.
“Sisi viongozi wa vyama vya siasa, hususan vyama vya upinzani, kwa muda mrefu, kwa miaka mingi, hasa kutokea mwaka 2000, tumepiga kelele sana kuhusu mikataba ya madini na namna maliasili zinavyoibiwa,” alisema.
Alisema itakuwa ajabu sasa wakianza kubeza juhudi hizo.
No comments