Breaking News

Mbowe Asikitishwa naa Kauli ya Kardinali Pengo Kuhusu Mchakato wa Katiba

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kauli ya Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuhusu mchakato wa Katiba imewasikitisha.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amesema kiongozi huyo wa dini anapaswa kulinda heshima aliyonayo ndani na nje ya kanisa.

Akizungumza na Mwananchi, Mbowe amesema, “Askofu Pengo ni kiongozi wa kanisa, anaheshimika na wananchi ambao si wale anaowaongoza lakini kwa kauli yake kuhusu Katiba, imetushangaza na imenisikitisha.”

Mbowe amesema, “Suala la elimu, chakula na maisha yetu yanalindwa na Katiba, ndiyo msingi wa mifumo ya rasilimali za Taifa. Anaposema haoni umuhimu wa Katiba anatufikirisha, anataka kusema mchakato wa Katiba uliogharimu mabilioni ya fedha leo hauna maana?”

Amesema umefika wakati mchakato wa Katiba uliokwama ukaendelezwa na hasa kuanzia katika rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya mwenyekiti, Jaji mstaafu Joseph Warioba.

“Katiba ni maridhiano, tunahitaji kupata maridhiano ya pande zote, nirudie tu kwamba alichokisema Askofu Pengo kinasikitisha,” amesema Mbowe.

Kardinali Pengo Jumamosi iliyopita alinukuliwa akisema kauli iliyotolewa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi kuwa Katiba mpya ndiyo kipaumbele cha wananchi ni maoni yake binafsi na si msimamo wa Kanisa Katoliki nchini.

Alisema hilo alipotoa ufafanuzi kuhusu  sitofahamu iliyojitokeza miongoni mwa Watanzania na waumini wa kanisa hilo kutokana na kauli ya Askofu Niwemugizi.

“Napenda kutamka moja kwa moja kwamba huo si msimamo wa kanisa na hauwezi kuwa msimamo wa kanisa kwa sababu sisi tuna utaratibu wetu wa kuishauri Serikali au kuzungumzia masuala ya jamii,” alisema.

Hivi karibuni Askofu Niwemugizi alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kipaumbele cha kwanza cha Watanzania ni Katiba mpya na kuongeza yeye binafsi ni miongoni mwa watu walioipinga Katiba Inayopendekezwa.

No comments