Breaking News

Kiongozi wa halmashauri awekwa ndani Tunduma

 Anakuwa kiongozi wa nane kukamatwa na kuwekwa mahabusu

 Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tunduma, Herode Jivava ametiwa nguvuni na Polisi akidaiwa kutishia kuua kwa maneno.

Jivava ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Songwe anakuwa kiongozi wa nane kukamatwa na kuwekwa mahabusu. Baadhi ya waliokamatwa  wamefunguliwa kesi mahakamani na wengine wako nje kwa dhamana wakisubiri upelelezi wa polisi kukamilika.

Akizungumza na Mwananchikuhusu kukamatwa kwa Jivava, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Mkoa wa Songwe, Ayub Sikagonamo amesema alikamatwa jana Jumapili jioni mjini Vwawa akijiandaa kuingia uwanjani kuangalia mpira na alipelekwa Kituo cha Polisi Tunduma.

“Asubuhi hii tumefika hapa Polisi tumeambiwa Jivava anatuhumiwa kwa kosa la kutishia kuua kwa maneno. Eti aliwatishia mgambo wakati wakiwaondoa kwa nguvu Machinga mjini Tunduma,” amesema.

 Sikagonamo amesema wanamsubiri mwanasheria ili kushughulikia suala hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange hakuwa tayari kuzungumzia taarifa za kukamatwa kwa Jivava akimtaka mwandishi wa Mwananchikusubiri ili afuatilie tukio hilo.

No comments