Breaking News

JUMAMOSI NI VITA YA AJIB NA OKWI NANI KUIBUKA MBABE


Miamba ya soka la Tanzania Yanga na Simba wanakutana Jumamosi hii kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa mzunguko wa nane kwa timu zote mbili.

Timu hizo zinakutana zikiwa zinalingana kwa poini Simba iliyopo kileleni kwa wingi wa mabao inapointi 15, sawa na Yanga ambayo inashika nafasi ya pili kutokana na uchache wa mabao ya kufunga.

Kama ilivyo kawaida ya mechi hiyo maarufu kama Dar Derby, kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka Tanzania nzima, hali hiyo imeendelea kama ilivyokuwa kawaida kwani hadi kufikia sasa kila upande unajitapa kuibuka na ushindi katika pambano hilo ambalo litachezeshwa na mwamuzi Elii Sasi ambaye ndiye aliyechezesha mchezo uliopita wakati timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.

Gumzo kubwa kuelekea mchezo huo ni washambuliaji Ibrahim Ajibu anayechezea Yanga akitokea Simba na Mganda Emmanuel Okwi, ambaye amekuwa na kasi nzuri ya ufungaji akifunga mabao nane katika mechi saba alizoichezea timu hiyo.

Mshindi katika mchezo huo ataongoza ligi kwa tofauti ya pointi na kuweka matumaini ya kufanya vizuri msimu huu, huku timu itakayofungwa huenda mambo ya kaanza kuharibika hapo na kuwa na msimu mbaya kama ilivyozoeleka.

Rekodi zinaibeba Simba, katika mchezo huo kwamba ina asilimia kubwa ya kushinda mchezo huo wa Jumamosi kutokana na ubora wa kikosi ilichokuwa nacho hivi sasa pamoja na ukali wa safu yake ya ushambuliaji ambayo imefunga idadi kubwa ya mabao ukilinganisha na Yanga.

Yanga haijawahi kuifunga Simba mechi tatu za mwisho, tangu ilivyofanya hivyo msimu wa 2015/16 iliposhinda mechi zote mbili za ligi kuu mambo yamekuwa tofauti msimu huu uliofuata ambapo licha ya kufanikiwa kutetea ubingwa wake lakini Yanga ilitoka sare mechi ya mzunguko wa kwanza na kufungwa mabao 2-1, katika mechi ya pili.

Lakini kabla ya hapo Simba iliifunga Yanga kwa penalti 4-3, kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi Visiwani Zanzibar, baada ya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

Mapema msimu huu Simba ilijiwekea rekodi nyingine kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, kwa kuifunga Yanga, kwa mikwaju ya penalti 5-4, baada ya kutoka sare kwenye muda wa kawaida.

Takwimu hizo ndizo zinazofanya mchezo ghuo kuwa mgumu kwani niwazi kuwa Yanga haitokubali kuendelea kuwa wanyonge kwa kikosi cha kocha Joseph Omog, ambaye tangu aanze kuifundisha Simba hajapoteza mchezo hata mmoja mbele ya Yanga.

Hiyo ni nafasi muhimu kwa kocha George Lwandamina ambaye katika mechi nne alizokutana na Simba hajashinda hata moja zaidi ya kupata sare moja na kufungwa tatu mfululizo.

Ukiacha vita ya Ajibu na Okwi, kwahiyo vita nyingine itakuwa upande wa makocha ambapo Lwandamina atakayekuwa mwenyeji wa mchezo huo akimkarisha Omog, ingawa makocha wote hawa wapo katika hatari ya kufukuzwa kwa atakayepoteza mchezo.

Mapambano makubwa katika mchezo huo yanatarajiwa kuwepo kwenye eneo la kiungo ambapo Haruna Niyonzima aliyekuwa Yanga atakuwa na kazi ya kumpita kiungo mpya wa Yanga Papy Kabamba Tshishimbi ambaye anaonekana kuziba vizuri eneo la kiungo mkabaji la Yanga.

Tshishimbi amekuwa na faida nyingi kwenye kikosi cha Yanga tangu alipotua anauwezo wa kukaba na kuichezesha timu jambo ambalo Niyonzima, hakuweza kufanya zaidi ya kushambulia na kutengeneza nafasi za mwisho.

Kwa kufuatilia mechi tatu za mwisho za timu zote mbili vikosi vya timu zote mbili vinatarajiwa kupangwa kama ifuatavyo

Simba inatarajia kumtumia Manula golini; mabeki wakiwa ni Earsto Nyoni, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’, Method Mwanjale na Juuko Murshid.

Viungo wataanza Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na Haruna Niyonzima na mbele yao wakicheza Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi na Laudit Mavugo.

Yanga ina asilimia kubwa ya kuanza na kikosi hiki; Rostand kama kawaida atakamata milingoti. Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’ na Kelvin Yondani wataunda safu ya ulinzi. Tshishimbi, Pius Buswita, Raphael Daud kisha washambuliaji wakasimama Ajibu, Chirwa na Geofrey Mwashiuya.

No comments