#JEZI YA NIYONZIMA KIGUGUMIZI MITANDAONI
Kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima.
BAADA ya kuibuka minog’ono ya muda mrefu kuhusu Kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima raia wa Rwanda, kutoposti picha kwenye mitandao yake ya kijamii akiwa na uzi wa Simba, nyota huyo ameibuka na kusema kuwa ametua katika klabu hiyo kwa kazi moja tu ya kucheza mpira.
Niyonzima ambaye amesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Yanga kwa dau la milioni 115, amefanikiwa kuichezea timu hiyo michezo minne ya ligi kuu hadi sasa huku akikosa mechi moja dhidi ya Mwadui kutokana na kuumwa malaria.
Aidha hivi karibuni, kulizuka mjadala katika mitandao ya kijamii kwa baadhi ya mashabiki wa Simba kuhoji kwa nini kiungo huyo hajaposti picha yake mpya akiwa na jezi ya timu yake hiyo ya sasa katika ukurasa wake wa Instagram.
Hata hivyo, Niyonzima ameonekana kuwajibu kwa vitendo mashabiki hao baada ya Ijumaa iliyopita kutupia picha yake akiwa na jezi ya Simba pamoja na wachezaji wenzake wakiwa mazoezini.
Championi Jumatano, lilimtafuta Niyonzima kuzungumzia suala hilo ambapo alisema kuwa, kwa upande wake ametua Simba kwa ajili ya kazi moja tu ya kuhakikisha anaitumikia ipasavyo klabu yake hiyo na si kutupia picha mitandaoni.
“Mimi nimetua Simba kwa kazi moja tu ya kuhakikisha naitumikia timu yangu ipasavyo, nashangaa ninavyosikia habari hiyo na wala sijui kinachoendelea, mimi nipo hapa kwa ajili ya kucheza na si kutupia picha mitandaoni japokuwa siwezi kujibu kiundani suala hilo na wala haiingii akilini,” alisema Niyonzima.
No comments