Breaking News

Familia ya Lissu yafanya kikao na Bunge


Familia imefanya kikao cha siri na uongozi ya Bunge kujadili matibabu ya mbunge huyo.

 Wakati Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi, familia yake imefanya kikao cha siri na uongozi ya Bunge kujadili matibabu ya mbunge huyo.

Kikao hicho kimefanyika leo Jumatatu jijini Dar es Salaam na imeelezwa kimehudhuriwa na Spika Job Ndugai, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, Mbunge wa Hanang’, Dk Mary Nagu na ndugu watatu wa Lissu, wanaume wawili na mwanamke mmoja.

Baada ya kupata taarifa za uwepo wa kikao hicho Mwananchiiliweka kambi nje ya Ofisi Ndogo za Bunge tangu saa 3:55 asubuhi na kushuhudia shughuli za kawaida zikiendelea huku kukiwa na watu wachache wanaoingia na kutoka ndani ya ofisi hizo.

Ilipofika saa 7:40 mchana, alitoka Mbatia akielekea kwenye gari lake baada ya kumaliza kikao hicho. Mwandishi alimfuata kujua kilichojiri ndani ya kikao hicho, Mbatia alikiri kuwepo kwa kikao hicho lakini hakutaka kuzungumza lolote na kuelekeza aulizwe Spika Ndugai.

“Ni kweli tulikuwa kwenye kikao na familia ya Lissu, lakini siwezi kusema tumezungumzia nini.  Kwa taarifa zaidi nendeni kwa Spika au Katibu wa Bunge, walikuwepo pia ndugu zake watatu, wafuateni wanaweza kuwaeleza,” alisema Mbatia.

Msemaji wa familia ya Lissu, Alute Mughwai alipotafutwa alisema kikao hicho kimefanyika kati ya familia na uongozi wa Bunge kuhusu mambo yanayomhusu Lissu, hata hivyo alisema hakijakamilika kwa sababu ya kukosekana kwa upande wa Chadema.

Mughwai alisema kikao hicho kimeahirishwa mpaka wakati mwingine pande zote zitakapotimia ili kulijadili suala hilo kwa ukamilifu wake. Alisema Chadema kupitia kwa mwenyekiti wake Freeman Mbowe walipewa mwaliko lakini hawakuweza kufika.

“Siwezi kukwambia tumezungumzia nini, moja ya masharti tuliyopeana ni kutokusema hadharani mambo tuliyoyajadili lakini yanamuhusu Lissu. Wote ‘interest’ yetu ni kuona Lissu anapona na kuendelea na majukumu yake kama kawaida,” alisema Mughwai.

Hata hivyo, jitihada za kumtafuta Spika wa Bunge pamoja na Katibu wa Bunge zilishindikana baada ya simu zao kuita bila kupokelewa.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alipoulizwa kuhusu kikao hicho amesema taarifa kuhusu kikao hicho zilipelekwa Ofisi ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na siyo kwenye chama.

No comments