Aliyesambaza Habari za Uongo Kuhusu Mazungumzo ya Serikali Wawakilishi wa Kampuni ya Acacia Apandishwa Kizimbani
Mkazi wa Chato mkoani Geita, Obadia Kiko (41), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook kuhusu mazungumzo kati ya Serikali na wawakilishi wa kampuni ya Acacia.
Wakili wa Serikali, Leonard Challo amedai mahakamani kuwa Agosti 3, 2017 huko Chato Geita mshtakiwa huyo alifanya kosa hilo kupitia mtandao huo wa kijamii wa Facebook.
Challo ametoa madai hayo leo Jumanne mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri. Mshtakiwa huyo anadaiwa kusambaza maneno kuwa "Taarifa kutoka kikao cha mazungumzo kati ya Serikali na wawakilishi wa kampuni ya Acacia kuwa wanasheria wa upande wetu wanashindwa kutafsiri baadhi ya vifungu vya sheria hadi kufikia kuomba msaada kwa wanasheria wa Acacia sasa huoni hivi ni vituko mwizi anakusaidia sheria haahaa haha."
Inadaiwa aliendelea kusambaza maneno kuwa, "mazungumzo bado yanaendelea lakini wanasheria wetu wamebanwa sana ukizingatia wale jamaa wana vielelezo vyote vya mikataba kiukweli tumuombe Mungu maana Serikali ikitaka kuvunja mkataba na Acacia gharama kubwa zitatuusu."
"Lakini pia kuendeleza uvyama utatugharimu saana, baada ya mh. Rais Magufuli angewashirikisha mawakili wasomi waliokwishaiva wakili Lissu, wakili Kibatara na Fatma Karume kwenye mambo ya umuhimu kama haya yeye kaleta uchama sasa itatugharimu .// Dicteta Magufuli mist go" . Maneno hayo yanadaiwa kusambazwa na mshtakiwa huyo kupitia mtandao huo wa kijamii wa Facebook.
Wakili Challo amedai kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo la kupotosha umma.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ukadai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Kwa upande wa Wakili Peter Kibatala anayemtetea mshtakiwa huyo aliomba mteja wake apatiwe dhamana na kwa masharti nafuu.
Wakili Challo alieleza kuwa hana pingamizi la dhamana.
Hakimu Mashauri alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaoamika ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh 5 milioni.
Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 16, 2017. Hata hivyo mshtakiwa huyo hakuwa na wadhamini.
No comments