Breaking News

YANGA YASAINI MKATABA NA AZAM

Kikosi cha timu ya Yanga.

KLABU ya Yanga, jana ilifanikiwa kuingia mkataba wa miaka mitatu na Kampuni ya Uhai Production Media Group, kwa ajili ya kurusha matangazo yake ya kipindi cha television ‘Yanga TV’ katika moja ya chaneli za Azam TV.

Kwa kusaini mkataba huo kwa Yanga inakuwa inaungana na mahasimu zao wakuu, Simba ambao tayari muda mrefu walikuwa wameingia makubaliano na kampuni hiyo kwa ajili ya kurusha kipindi chake katika Simba TV.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, amekiri kusaini mkataba wa miaka mitatu na Azam TV ambapo sasa utaipatia fursa klabu hiyo ya kuongeza kipato kupitia Azam TV, tofauti na hapo mwanzo ambapo hawakuweza kufikia mwafaka.

“Ni kweli tumesaini mkataba wa kurusha matangazo yetu Azam TV, japo siyo suala geni sana kwetu kwani huko mwanzo tuliwahi kufanya nao mazungumzo kabla hata ya Simba ambao wao waliingia nao makubaliano kipindi hicho.

“Tumefanya hivi kwa maana nzuri ya kuiongezea kipato klabu yetu ambapo tumekubaliana kuwa mkataba huu utakuwa ukidumu ndani ya miaka mitatu mitatu na baadaye tutakuwa tukikaa mezani na kuupitia upya kulingana na mahitaji ya kipindi hicho yatakavyokuwa.

“Huko nyuma hatukuweza kufanya hivyo kutokana na hali halisi ya uongozi wa juu kutoafikiana ila kwangu mimi ninalazimika kupanua wigo wa pato la klabu ili iweze kujiendesha yenyewe pasipo kuwa tegemezi.

“Ndiyo maana utaona napambana na wenzangu kufungua vyanzo vingi vya mapato kwa lengo la kuifanya ikidhi baadhi ya mahitaji ambayo yamekuwa changamoto kwetu,” alisema Sanga ambaye anakaimu nafasi ya uenyekiti iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa mwenyekiti, Yusuf Manji kujiuzulu.

No comments