MBOWE;LISSU MZIMA LAKINI HALI YAKE SIO NZURI
Mbowe yuko na Lissu jijini Nairobi akifuatilia matibabu ya mbunge huyo wa Singida Mashari aliyepigwa risasi jana
Nairobi. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Tundu Lissu ni mzima lakini yuko katika hali ambayo si nzuri.
Lissu ambaye alisafirishwa jana usiku kwenda Kenya kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi mjini Dodoma amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan Nairobi.
Mbowe alieleza kuwa kabla ya shambulio hilo alikutana na Lissu na wakapata chakula cha mchana pamoja baada ya hapo kila mmoja aliendelea na mambo yake hadi pale alipopigiwa simu za taarifa ya tukio hilo.
Alisema hafikirii kama wahuni ndiyo waliofanya shambulio hilo kwani Lissu hana maadui nje ya siasa.
“Tunashuku kuna msukumo wa kisiasa katika shambulio hili ikizingatiwa silaha nzito iliyotumika, idadi ya risasi zilizofyatuliwa ni wazi wahusika walikuwa na nia ya kumuua na sio kumuibia au kuchukua chochote kutoka kwake,”
"Kama wengi wezi au wahuni angalau wangeiba laptop yake au vitu vingine vya thamani. Ukiangalia idadi ya risasi zilizofyatuliwa ni kiashiria kuwa ni shambulio la kisiasa.”
Mbowe alisema hawafikirii kama raia wa kawaida ndiyo wamehusika kwenye shambulio hilo ila huenda maadui wake kisiasa ndiyo wanaweza kuhusika.
“Hatutamtuhumu yeyote kuhusika na shambulio hilo ila iko wazi kabisa kwamba maadui wake kwenye siasa ndiyo wamehusika.”
Alisema, “Ingawa hii ni mara ya kwanza kwa mmoja wetu kupigwa risasi, tunaona huu ni mwendelezo wa vitendo vya unyanyasaji tunavyofanyiwa kwa kuikosoa Serikali. Kuwa mwanasiasa wa upinzani si salama tena Tanzania,”
Akitolea mfano matukio ya wabunge na viongozi wa upinzani kukamatwa na polisi na kunyimwa dhamana na kufutiliwa maandiko yao kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo kiongozi huyo alisema katu wanachama wa chama chake hawataogopa kupaza sauti na wataendelea kupambana kuhakikisha demokrasia inasimama Tanzania.
Kufuatia hali hiyo mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Kenya, Erioc Mutua ameiomba serikali ya Kenya kumpatia ulinzi Lissu wakati akiwa hospitalini hapo.
“Hatuna uhakika watu waliotaka kumuua Tanzania, hawatafikiria kuja hapa kutimiza lengo lao. Ni muhimu kwa serikali kuweka askari watakaomlinda kuhakikisha anakuwa salama,”alisema Mutua
No comments