WABUNGE KUPIMWA VVU BUNGENI
NAIBU Spika, Dk. Tulia Ackson, amemwomba Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kupeleka vipimo vya Ukimwi, ili wabunge waweze kupima na kujua hali zao.
Dk. Tulia aliyasema hayo jana baada ya kipindi cha maswali na majibu alipokuwa akijibu miongozo mbalimbali iliyoombwa na wabunge.
Majibu hayo ya Naibu Spika yalitokana na mwongozo wa Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Josephat Kasheku maarufu kama Musukuma, aliyetaka kupata ufafanuzi wa kauli iliyotolewa na Waziri Ummy wakati akijibu maswali.
Musukuma alisema kauli ya Waziri Ummy kuwataka wanaume wote wameze dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARV), itawaweka kwenye wakati mgumu hivyo kutaka ufafanuzi.
“Mheshimiwa Naibu Spika wakati Waziri Ummy anajibu swali bungeni leo alisema kuwa wanawake wengi wanameza ARVs, lakini wanaume wengi hawamezi hivyo kuwahamasisha wanawake wawahimize wanaume wote kunywa hizi dawa,” alisema.
“Sasa mheshimiwa Spika naomba ufafanuzi maana Waziri anaposema wanaume wote tunywe zile dawa unamaanisha nini maana kauli hii inaweza kutuletea shida sisi wanaume.”
Akijibu mwongozo wa Mbunge huyo uliosababisha wabunge wote kuangua kicheko, Naibu Spika alisema waziri alikuwa akimaanisha kuwa idadi kubwa ya wanawake wenye VVU wanatumia dawa za ARV hivyo kuwataka wawahamasishe wanaume zao nao wazitumie, ili kurefusha maisha.
“Mheshimiwa Mbunge hili mbona liko wazi," alisema Dk. Tulia.
Aidha, alimweleza Waziri Ummy kuwa hana uhakika kama takwimu alizotoa za watumiaji wa dawa za ARV zinahusisha na wabunge na kama haziwajumuishi basi ni muda wa kupeleka vipimo, ili nao wajue hali zao.
No comments