ODINGA AITISHA MAANDAMANO KUSHINIKIZA BABADILIKO IEBC.
Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, umesema siku ya Jumanne utaongoza maandamano ya wafuasi wake nje ya Ofisi ya Tume ya Uchaguzi jijini Nairobi, kushinikiza mabadiliko ndani ya Tume hiyo kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi mpya wa urais tarehe 26 mwezi Oktoba.
Kiongozi wa muungano huo Raila Odinga ametangaza kuwa, hawatakubali kufanyika kwa Uchaguzi huo iwapo Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Ezra Chiloba na maafisa wengine wataendelea kuandaa uchaguzi mpya.
Naibu rais William Ruto ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha Jubilee ameshutumu kauli ya Odinga na kueleza ni mbinu ya kiongozi huyo wa upinzani kutotaka Uchaguzi.
Mvutano wa kisiasa unaendelea nchini Kenya, huku ikiripotiwa kuwa Tume ya Uchaguzi inapanga kukutanana wawakilishi wa pande zote mbili za kisiasa, kukubaliana kuhusu maandalizi ya Uchaguzi mpya.
Wakati uo huo, kiongozi wa mashtaka nchini Kenya Keriako Tobiko, ameagiza kuchunguzwa kwa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya baada ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi wa urais mwezi uliopita.
Tobiko ameagiza Polisi na maafisa wa tume ya kupambana na ufisadi kuchunguza iwapo wafanyikazi wa Tume hiyo waliohusika na udanganyifu uliosababisha matokeo hayo kufutwa.
No comments