Breaking News

MAPACHA WALIOUNGANA WAANZA MASOMO YA CHUO


Pacha walioungana Maria na Consolata wamewasili katika Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Ruaha (Rucu) kujiandaa kwa masomo ya shahada ya elimu.

Wamesema leo Jumatano kuwa wamefurahi na wanaushukuru uongozi wa chuo na wanafunzi kwa kuwapokea kwa furaha na kuwaandalia mazingira mazuri ya kusomea na kuishi.

Pacha hao wamesema wamewasili mapema chuoni kwa sababu wanataka kujifunza kompyuta ili waendane na spidi ya wanafunzi wengine.

Kwa mujibu wa pacha hao, ndoto yao ya kufika chuo kikuu imetimia, hivyo wanalishukuru shirika la wamisionari la masista wa Consolata kwa kuwalea na kuwapa moyo. Pia wamewashukuru wafadhili waliojitolea kuwalea mpaka walipofikia.

Mtawa Consolata kutoka shirika hilo, amesema wamewawahisha chuoni ili wajifunze kompyuta iwasaidie katika masomo yao.

“Sisi tuliwatunza tukiwa Kilolo, hapa watatunzwa na masista wa Teresia ambao wamewaandalia mazingira mazuri ya kuishi kama walivyoomba. Tumeridhika na tunawatakia kila la heri. Tutakuwa tunakuja kuwaona mara kwa mara,” amesema sista Consolata.

 Pacha hao wameandaliwa vyumba vitatu, jiko, sebule na maliwato inayojitegemea ndani ya chumba chao.

Makamu Mkuu wa Chuo (Fedha na Utawala), Padri Kelvin Haule amesema wanajisikia vizuri kuwapokea pacha hao.

Amesema masomo yao ya elimu ya juu yanaanza mwishoni mwa Oktoba lakini masomo ya kompyuta yataanza kesho.

Mwalimu wa kompyuta katika Chuo cha Rucu, Robert Manase amesema atahakikisha anawasaidia.

“Maria na Consolata wanafahamu kidogo kompyuta lakini kutokana na mazingira yao nitahakikisha wanajua zaidi kwa sababu wameamua kuja mapema kusoma,” amesema.

No comments