MAGHEMBE AWASHA MOTO HIFADHI YA ARUSHA
Waziri wa Maliasili, Profesa Jumanne Maghembe akiwa ziarani katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha kukagua shughuli za uhifadhi. Picha na Ofisi ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Profesa Maghembe ameagiza wote waliolima ndani ya hifadhi waondoe mazao yao.
Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameagiza wote waliolima ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha kinyume cha sheria waondoe mazao na kusitisha shughuli zozote za kibinadamu kwenye eneo la hifadhi.
Profesa Maghembe ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), kupitia hifadhi hiyo kuhakikisha hilo linatekelezwa.
"Ni marufuku mtu yeyote kuonekana akilima katika eneo hili, wekeni askari hapa, atakayeonekana piga pingu, hatuwezi kushuhudia watu wanalima ndani ya hifadhi tukae kimya, ni lazima tuchukue hatua. Watangaziwe na wapewe muda wa kuondoa mazao yao, ndani ya siku 30 au 40 wawe wameshaondoka," ameagiza waziri.
Agizo hilo amelitoa akiwa ziarani katika hifadhi hiyo iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha kukagua shughuli zinazofanywa na hifadhi, ikiwemo maeneo yenye mgogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.
Awali, akiwasilisha taarifa kwa waziri, Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga amesema eneo hilo ambalo pia linajulikana kama shamba namba 40 na 41 limekuwa na mgogoro tangu mwaka 1990 baada wananchi wa Kijiji cha Olkung'wado kulivamia wakitoa hoja kadhaa, ikiwemo madai kuwa ni maeneo yao ya asili waliyoyamiliki tangu zamani.
Amesema hoja nyingine wanazozitoa wananchi ni kuwa, walipewa mashamba hayo na Serikali wakati wa operesheni ya uanzishwaji wa vijiji mwaka 1975 na 1976.
Pia, wanadai hawakushirikishwa kwenye mchakato wakati wa ugawaji wa mashamba hayo na Tanapa haina hati miliki ya mashamba hayo.
Ngada amesema hoja hizo zinakinzana na ukweli kuwa, shamba hilo lilimilikishwa kwa Tanapa mwaka 1980 baada ya kutolewa tangazo kwa wadau wanaoweza kuliendeleza kutokana na mwekezaji wa awali kushindwa kuliendeleza, hivyo kufutiwa hati miliki na Rais mwaka 1979.
Amesema wadau kadhaa waliomba umiliki wa shamba hilo ikiwemo Halmashauri ya Kijiji cha Olkung'wado, lakini Kamati ya Ushauri ya Ardhi ya Mkoa wa Arusha ikaishauri Serikali mashamba hayo yamilikiwe na Tanapa, hivyo waliandikiwa barua ya kukubaliwa kupewa shamba na Idara ya Ardhi Mkoa.
Hata hivyo, amesema katika kikao cha wadau wa uhifadhi kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mei 11 iliazimiwa na kuridhiwa na Bodi ya Wadhamini ya Tanapa kuwapa wananchi eka 366 ya shamba hilo na kubakiwa na eka 600.
“Kikao pia kiliridhia Tanapa kuweka vigingi vya mpaka katika shamba hilo, Mei 14 zoezi hilo lilianza na jumla ya vigingi 26 viliwekwa,” amesema.
Hata hivyo, amesema kumekuwepo taarifa kuwa baadhi ya wanakijiji wa Kitongoji cha Momella walifungua kesi mahakamani wakidai Kijiji cha Olkung'wado kimenyang'anywa ardhi na Tanapa.
Amesema Serikali ya kijiji imekana kwa maandishi kuhisika na ufunguzi wa kesi hiyo ikisema imefunguliwa na mtu binafsi.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Dk Allan Kijazi amesema maagizo yote aliyoyatoa waziri ya kusitisha shughuli za kibinadamu ndani ya eneo hilo yatafanyiwa kazi na atapewa mrejesho wa utekelezaji wake.
No comments