Korea Kaskazini yafyatua kombora kupitia anga ya Japan
Seoul, Korea Kusini. Korea Kaskazini imeuthibitishia ulimwengu kwamba haitishwi na taifa lolote wala vikwazo ilivyowekewa baada ya jana kufyatua kombora la masafa marefu kupitia anga ya kisiwa cha Hokkaido, Japan.
Taifa hilo la kijamaa limefyatua kombora hilo siku moja baada ya kutishia kuizamisha Japan na kuiangamiza Marekani ibaki “majivu na giza” kwa kuliunga mkono Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekewa vikwazo vya kiuchumi baada ya kufanya jaribio la nyuklia Septemba 3.
Naibu waziri wa ulinzi wa zamani wa Marekani, Lawrence Korb katika uchambuzi wake aliiambia televisheni ya Al Jazeera kwamba jaribio hilo halikushtua kwani mara zote Korea Kaskazini inataka kuonyesha hasira zake dhidi ya vikwazo ilivyowekewa.
"Kimsingi tulijua kwamba Korea Kaskazini itafanya jambo fulani kwa sababu walikuwa wanapeleka vifaa eneo wanalofyatulia makombora. Ni wazi kwamba jaribio hili lilikuwa la kuonyesha ukaidi wake,” alisema.
Jeshi la Korea Kusini linasema kuwa kombora hilo limefyatuliwa kutoka maeneo ya karibu na mji mkuu wa Pyongyang.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson ametoa wito kwa China na Urusi kuchukua hatua za moja kwa moja dhidi ya Korea Kaskazini, huku Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe akitaja jaribio hilo kuwa ni kitendo cha kuudhi.
“China na Urusi lazima zionyeshe kwamba zimechoshwa na hatua ya Korea Kaskazini kuendelea kufanyia majaribio makombora yake kwa kuichukulia nchi hiyo hatua ya moja kwa moja,” alisema Tillerson. China huiuzia Korea Kaskazini mafuta na Urusi ndiyo taifa lililowaajiri raia wengi wa Korea Kaskazini.
Waziri wa Nchi Mratibu wa Sera, Yoshihide Sug amesema, "Japan tunapinga kwa nguvu zetue zote urushwaji wa kombora hilo na tutachukua hatua stahiki na kwa wakati kwenye Umoja wa Mataifa na kwingineko huku tukishirikiana na Marekani na Korea Kusini," alisema Suga.
Korea Kusini
Dakika chache baada ya ufyatuzi huo Korea Kusini ilifyatua makombora mawili ya masafa marefu baharini katika hatua ya kuionya Korea Kaskazini kulingana na chombo cha habari cha Yonhap.
Rais Moon Jae-in alifanya kikao cha dharura na kuonya kwamba kombora hilo litasababisha vikwazo zaidi dhidi ya Korea Kaskazini.
No comments