Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Kimemtaka Rais Magufuli Kufanyia Marekebisho Sheria ya Adhabu ya Kifo
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimemtaka Rais John Magufuli kuanzisha mchakato wa kuifanyia marekebisho sheria inayotoa adhabu ya kifo.
Akizungumza leo Jumanne, Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema wamefurahishwa na kauli ya Rais Magufuli kwamba hawezi kusaini hukumu ya kifo.
Rais Magufuli alionyesha kutofurahishwa na adhabu hiyo jana Jumatatu wakati wa hafla ya kumwapisha Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma.
Dk Kijo Bisimba amesema kwa kuwa Rais haipendi adhabu hiyo, hata Watanzania wengine hawaipendi pia.
Amesema Rais atumie nafasi yake kusimamia mchakato wa kurekebisha sheria na adhabu hiyo.
Mkurugenzi huyo amesema hata marais wa Serikali za awamu ya tatu na nne Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete hawakusaini ili kutoa adhabu ya kifo.
Amesema pamoja na kutosaini lakini hawakusema kuwa hawaipendi adhabu hiyo.
"Tunamshukuru Magufuli angalau ameonyesha kutoipenda adhabu ya kifo, sasa aifanyie marekebisho sheria," amesema.
No comments